Magugu maji ni kula yangu, ni mtaji wangu - Mariama Mamane

30 Julai 2019

 Ili kutatua changamoto kubwa zinazoikabili dunia hivi sasa kuanzia umaskini, mabadiliko ya tabianchi na hata majanga ya asili tunahitaji utashi, hatua zaidi na hatua zenyewe zichukuliwe sasa. Kauli hiyo imetolewa na bingwa kijana wa mwaka  2017 wa kupigania maslahi ya dunia Mariama Mamane kutoka Burkina Faso. Tupate maelezo zaidi na Jason Nyakundi

Ougadougou Burkina Faso bingwa huyo wa maslahi ya dunia anasema suluhu kwake yeye ni kugeuza changamoto hizo zinazoikabili dunia na kuwa fursa kubwa katika jamii kama alivyofanya yeye akianza kwa kujitambulisha, "mimi ni Mariama Mamane ni mwanzilishi na meneja mkuu wa mradi wa Jacigreen nambadili magugumaji kuwa nishati kwa wote “

Mradi wa Mariama ambao ni wa majaribio mbali ya kuzalisha nishati pia unatumia magugu maji hayo kuzalisha mbolea ya asili, unazuia hali ya jangwa, uhakikisha uhakika wa chakula na kuzalisha umeme utokanao na gesi ya samadi. Na sio tu unampatia kipato lakini pia umeinusuru jamii yake mfano mbolea wanayotengeneza akisema kuwa, “inasaidia uzalishaji wa kilimo na inahitaji nafasi ndogo kuweza kuzalisha mazao mengi, leo hii kutokana na mradi huu tunaweza kukidhi mahitaji ya kaya zaidi ya 12,000 na wakulima zaidi ya 100, ambao wataweza kutumia mbolea yetu.”

 Kwa mujibu wa Mariama ndoto yake ilitimia pale alipotunukiwa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya kuwa bingwa kijana wa kutetea maslahi ya dunia 2017.

Mariama anasema kuwa, “tuzo hii ilinitambulisha kimataifa na kuniwezesha kufadhili mradi wangu leo hii na lengo langu ni kuchagiza wasicha wengine kama mimi kupigania mustakabali wetu, ninataka kufanya kazi kutatua changamoto za kesho.”

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud