Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Papa Francis ataka silaha ziwekwe chini, na wanaopora mali waondoke

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis (kushoto) akiwa na Rais wa DRC  Felix-Antoine Tshisekedi jijini Kinshasa tarehe 31 Januari 2023
Ofisi ya Rais
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis (kushoto) akiwa na Rais wa DRC Felix-Antoine Tshisekedi jijini Kinshasa tarehe 31 Januari 2023

DRC: Papa Francis ataka silaha ziwekwe chini, na wanaopora mali waondoke

Amani na Usalama

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis aliyeko ziarani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amewasihi wakristo waweke silaha chini na badala yake wakumbatie huruma ya Mungu nchini humo. Radio Okapi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO imesema Papa Francis amesema hayo leo  wakati akihubiri kwenye misa iliyofanyika leo kwenye eneo la Ndolo, kitongoji cha Barumbu kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshasa. 

Wekeni silaha chini sakeni huruma ya Mungu 

"Wapendwa, siku hii iwe wakati wa neema ya kukaribisha na kuishi kwenye ungamo la Yesu Kristo,” amesema Papa Francis kwenye misa hiyo iliyohudhuriwa na takribani watu milioni mbili. 

Papa Francis ameendelea kusema, “siku hii iwe fursa ya kwenu ninyi ambao mnabeba mzigo mkubwa kwenye nyoyo zenu, kuondokana nayo na muanze kupumua upya. Hebu na kuweko na fursa ya kukiri kuwa ninyi ni wakristu ndani  ya taifa hili na mnafanya ghasia. Kwenu ninyi, Bwana anasema : Wekeni silaha chini na kumbatieni huruma ya Mungu.” 

Ametumia fursa hiyo kusihi walioshiriki misa hiyo kujikabidhi kwa Yesu Kristo ambaye kwa mujibu wake, anataka wakristu waweke madonda yao kwenye madonda yake. 

Nawasihi nayi mbebe misalaba yetu ili muweze kushirikisha madonda yenu na yale ya Yesu Kristo,” amesisitiza Papa Francis. 

Clémence Ndabohweje, mwenye umri wa miaka 49, akisafisha vyombo nje ya makazi yake kwenye kambi ya wakimbizi ya ndani ya Kanyaruchinya huko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC kufuatia mashambulizi ya M23. Anaishi hapa yeye na watoto wake 6 na waj…
UNICEF/Arlette Bashizi
Clémence Ndabohweje, mwenye umri wa miaka 49, akisafisha vyombo nje ya makazi yake kwenye kambi ya wakimbizi ya ndani ya Kanyaruchinya huko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC kufuatia mashambulizi ya M23. Anaishi hapa yeye na watoto wake 6 na wajukuu watatu.

Ondoeni mikono yenu DRC, ondoeni mikono yenu Afrika 

Mapema jana Jumanne baada ya kuwasili DRC Papa Francis alilakiwa na Rais Felix-Antoine Tshisekedi na baada ya hotuba ya Rais huyo, Papa Francis alizungumza na kutaka mataifa ya kigeni na mashirika ya kimataifa yanayopora rasilimali yaondoe mikono ya DRC halikadhalika barani Afrika. 

“Nchi hii imeporwa kwa kiasi kikubwa, haiwezi kunufaika na rasilimali zake zilizojaa tele: tumefikia kwenye utata ambapo matunda ya ardhi yake  yanakuwa ni ‘ya kigeni’ kwa wananchi wake. Sumu ya uchoyo imetia damu almasi yake. Ni janga ambamo kwalo kwa kiasi kikubwa nchi zilizoendelea kiuchumi zinafumbia macho, masikio na mdomo. Lakini nchi hii na bara hili wana haki ya kuheshimiwa na kusikilizwa,” amesema Papa Francis. 

Papa Francis amesisitiza, “acheni kuichafua Afrika: sio mgodi wa kunyonywa au ardhi kuibiwa rasilimali zake. Afrika iwe mhusika mkuu wa hatima yake.” 

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amesema  baada ya ukoloni wa kisiasa sasa Afrika inatawaliwa kiuchumi na hiyo lazima ikome. 

Taswira ya wananchi wa DRC ni kama jamii ya kimataifa imejiengua 

“Ukitazama hawa watu, mtu anaweza kudhani kuwa jamii ya kimataifa imejitoa katika vurugu inayowamaliza,” amesema Papa Francis na hiyo ametoa wito wa  

matumizi ya diplomasia kati ya mtu na mtu, baina ya watu na watu ambapo  kitovu chake kiwe ukuaji na maendeleo ya wananchi na si kujikita katika udhibiti wa maeneo au rasilimali za DRC ili hatimaye manufaa yawe kwa wananchi wote.