Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto za huduma za afya zimechochea usafirishaji haramu wa vifaa tiba Sahel: UNODC

Bidhaa bandia za matibabu.
Photo: WHO/Jim Holmes
Bidhaa bandia za matibabu.

Changamoto za huduma za afya zimechochea usafirishaji haramu wa vifaa tiba Sahel: UNODC

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti dawa na uhalifu UNODC imesema katika Ukanda wa Sahel changamoto za kupata huduma za afya zimechochea usafirishaji haramu wa vifaa tiba katika Ukanda huo.

Kwa mujibu wa ripoti ya ofisi hiyo iliyotolea Jumanne mjini Vienna, katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara vifo vipatavyo 267,000 kwa mwaka vinahusishwa na matumizi ya dawa za malaria ambazo ni batili au zisizo na viwango.

UNODC imeongeza kuwa na vifo vingine takriban 169,271 kwa mwaka vinahusishwa na dawa batili na viuavijasumu au antibiotic zinazotumika kutibu homa kali ya kichomi kwa watoto.

Ripoti inasema nchi za Ukanda wa Sahel na nchi za jirani zenye kiwango cha juu cha magonjwa ya kuambukiza ikiwemo malaria zinakabiliwa na changamoto hasa za upatikanaji na uwezo wa kumudu kufikia huduma za afya na hivyo kuweka mazingira ambayo mahitaji ya vifaa tib ana huduma kutokidhiwa kupitia mifumo ya kawaida wa huduma za afya.

Hivyo ripoti inasema pengo hilo baina ya mahitaji na usambazaji wa bidhaa za dawa zinazodhibitiwa hutoa fursa kwa biashara haramu, hutoa fursa ya motisha kwa vikundi vya uhalifu wa kupangwa na huchochea tishio linaloendelea kwa usalama wa umma na afya ya umma katika nchi za Sahel.

Ripoti hiyo ya UNODC inasema kati ya Januari 2017 na Desemba 2021 angalu tani 605 za bidhaa mbalimbali za matibabu zilizkamtwa Afrika Magharibi wakati wa operesheni za kimataifa.