Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yakabiliana na mahitaji ya dharura ya kiafya kusini mwa Libya

Mkimbizi kutoka Sudan akisubiri matibabu katika kituo cha afya cha UNHCR Tripoli, Libya
UN OCHA/GILES CLARKE
Mkimbizi kutoka Sudan akisubiri matibabu katika kituo cha afya cha UNHCR Tripoli, Libya

WHO yakabiliana na mahitaji ya dharura ya kiafya kusini mwa Libya

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limewasilisha dawa za matibabu kwa ajili ya watu takriban 400 wanaohitaji tiba dhidi ya kiwewe katika kituo cha afya cha Sabha, hospitali kuu ya Murzuq na hospitali ya Ghodwa. WHO imetoa pia vifaa vya kuwapatia joto watoto njiti pamoja na visafisha hewa katika kitengo cha watoto wachanga.

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO, mapigano katika ya makundi yaliyojihami Februari yalisababisha ongezeko ya majeruhi, na kusababisha vituo vya afya kuzidiwa uwezo wakati huu ambapo vimepungukiwa idadi ya wataalam na vifa tiba. Jumla ya majeruhi ni 250, ikiwemo watu 44 waliopoteza maisha na majeraha 2016.

Mnamo Februari, WHO imejiunga na ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa Sabha ambako imezindua sekta ya kitaifa kwa ajili ya kusimamia shughuli za kiafya ambapo kwa ushirikiano na taasisi za serikali na kituo cha kudhibiti magonjwa cha taifa wamekubaliana kuimarisha program ya kitaifa kuhusu kifua kikuu na ukimwi.

WHO imesaidia kituo cha taifa kutoa mafunzo na kuwasilisha timu za kukabiliana na milipuko ya magonjwa. Aidha WHO imepeleka mtaalamu wa saikolojia kutoa huduma kwa wagonjwa wa akili katika maeneo ya Sabha, Murzuq, Ghat na Ubari kwa ajili ya kutoa huduma maalum na kuimarisha hospitali nne kuu katika maeneo hayo.

Ili kuhakikisha huduma ya afya inapatikana kwa wote katika maeneo ya mahitaji, WHO inatekeleza huduma ya msingi katika maeneo ya Ash Shatti na Ubari kusaidia hospitali mbili na vituo vya afya tano na dawa muhimu, vifaa tiba, vifaa vya maabara na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya.