Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu umetekelezwa Unity:OHCHR/UNMISS

Wanawake wakitoka kuchukua kuni jimbo la Unity nchini Sudan Kusini ambayo imeshuhudia ukatili wa kijinsia.
©UNFPA South Sudan
Wanawake wakitoka kuchukua kuni jimbo la Unity nchini Sudan Kusini ambayo imeshuhudia ukatili wa kijinsia.

Ukatili na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu umetekelezwa Unity:OHCHR/UNMISS

Haki za binadamu

Ripoti ya pamoja ya haki za binadamu iliyochapishwa leo na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) na Ofisi ya kamishna mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) imeaanisha ukatili na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na ubinadamu kwenye jimbo la Unity Sudan Kusini.

Ukiukaji huu ulifanyika wakati wa mapigano kati ya vikosi vya pamoja vya Serikali na vikundi vya wanamgambo vinavyoshirikiana na serikali kwa upande mmoja, na wanachama wa Sudan People's Liberation Movement Army (SPLM/A-IO (RM)) kwa upande mwingine ambao ni watiifu kwa Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar.

Mapigano katika Jimbo la Unity kusini mwa nchi hiyo yaliathiri takriban vijiji na makazi 28  huku takriban raia 173 wakiuawa, 12 kujeruhiwa, na wanawake na watoto 37 kutekwa nyara.

Wengi wa waliotekwa nyara walifanyiwa ukatili wa kingono, wakiwemo wasichana wenye umri wa miaka minane na msichana wa miaka tisa ambaye alibakwa na kundi la watu wengi hadi kufa. Jumla ya kesi 131 za ubakaji na ubakaji wa genge zimerekodiwa na takriban raia 44,000 walikimbia makazi yao kutoka angalau vijiji 26.