Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwelekeo wa dunia katika kutegemea washawasha, senene na wadudu wengineo kama milo yenye virutubisho vingi

Wadudu lishe ambao wanaliwa na binadamu.
FAO
Wadudu lishe ambao wanaliwa na binadamu.

Mwelekeo wa dunia katika kutegemea washawasha, senene na wadudu wengineo kama milo yenye virutubisho vingi

Tabianchi na mazingira

Je umewahi kufikiria kuwa wadudu lishe ni moja ya majawabu ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, halikadhalika lishe na kutokomeza umaskini? Kama hapana, basi fuatilia makala hii kutoka mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo duniani, IFAD.

Kilimo kinaongoza kwa kusababisha mabadiliko ya tabianchi na wakati huo huo ni sehemu ya majawabu ya kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Wakulima wadogo na mabadiliko ya tabianchi

Wakulima wadogo ndio wana nafasi kubwa katika kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa sababu wao hawatumii mbolea hatarishi au pembejeo za kilimo kama vile mashine zinazotumia mafuta kisukuku, moja ya vyanzo vya utoaji hewa chafuzi.

Na ndio maana katika mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP27 Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya kilimo duniani, IFAD na Marekani, walizindua Ubia wa ahadi za kudhibiti utoaji wa hewa ya Methani duniani.

Ubia huu unalenga kusaidia wakulima katika nchi zinazoendelea kupunguza zaidi utoaji wa hewa chafuzi kama Methani na wakati huo huo kuhimili au kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Wadudu lishe kama senene na nyenje

Moja ya majawabu ya changamoto hiyo ni uzalishaji wa wadudu lishe. Wadudu hawa ni mlo kwa binadamu na wanyama.

IFAD katika chapisho lake inasema wadudu ni chanzo bora za protini, na madini na uzalishaji wake unaweza kufanyika bila kutoa kiwango kikubwa cha hewa chafuzi kwa mazingira.

Kiwango cha uzalishaji ni kikubwa na kwa kipindi kifupi na uzalishaji wake hauhitaji eneo kubwa au maji mengi.

Washawasha hawa wana kiwango kikubwa cha protini wanaitwa kwa kiingereza mopane caterpillar.

Takribani watu bilioni 2 duniani wanakula wadudu

Wadudu ni chanzo muhimu cha chakula kwa takribani watu bilioni 2 duniani, lakini katika nchi za magharibi ni zama hizi ambapo mataifa hayo yameanza kutathmini nafasi ya wadudu katika mifumo yao ya chakula.

Kwa kuzingatia gharama ndogo ya uzalishaji na nafasi ndogo inayohitajika, hata kwa watu maskini wanaweza kukusanya, kufuga, kuchakata, kuuza na kula wadudu.

IFAD inasema, “kukiwa na zaidi ya aina 2,000 za wadudu wanaoweza kuliwa na binadamu na wanyama, kuanzia nyenje, washawasha, hadi senene—kuna aina nyingi sana ya wadudu watamu ambao tunaweza kuchagua.”

Kwa mujibu wa chapisho la FAO, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC washawasha huchangia asilimia 40 ya protini inayotakiwa na binadamu. Washawasha anayeliwa zaidi barani Afrika anatambulika kwa kiingereza kama mopane caterpillar.

Wakati kula wadudu pekee hakuwezi kuwa jawabu la kutatua madhara ya mabadiliko ya tabianchi, uamuzi huu wa kubadili mlo unaweza kupunguza shinikizo la madhara ya tabianchi kwenye mazingira, na wakati huo huo mlo bora unaingia kwenye miili ya binadamu.

Kwa nini kula wadudu kunasaidia mwili wa binadamu?

  • Takribani asilimia 80 ya mwili wa mdudu umeumbwa na protini na virutubisho, ambapo protini yake inazidi ile ya mnyama afugwaye.
  • Wadudu wana kiwango kidogo cha mafuta, wanga na wamesheheni vitamini, madini na makambakamba au fibre kwa kiingereza.
  • Minyoo nayo ina kiwango sawa cha Omega-3 kama kwenye samaki.
  • Wadudu hawaambukizi magonjwa kwa binadamu na wanyama kama ilivyo kwa wanyama.

Kampuni zimeanza kutumia fursa

Baadhi ya kampuni zimeanza kuzalisha na kusindika wadudu kuwa unga kwa ajili ya chakula cha wanyama huku kampuni nyingine zikihamasisha watu juu ya faida za binadamu kuwa wadudu.

Miongoni mwa kampuni hizo ni Brooklyn Bugs ambayo imeanzishwa na Mpishi Mkuu wa Mpango wa IFAD wa Mapishi kwa Mabadiliko, Joseph Yoon.

Yoon anasema lengo la kampuni yake ni kuondoa uoga walio nao watu katika kula wadudu. “Tunataka kusaidia watu waondokane na uoga wa kile wasichokifahamu na kuwaonesha kuwa kikwazo kinachokuweko ni fikra ya kutofahamu jinsi ya kuwaandaa.”

Kadri mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri usambazaji na upatikanaji wa chakula, wadudu lishe nao wanaonekana kuwa eneo na jawabu bora kadri idadi ya walaji inavyoongezeka.

IFAD inasema punde maduka makubwa ya vyakula yataanza kuuza wadudu waliosindikwa na kufungwa kwenye paketi.