Chonde chonde hebu tujikwamue kutoka kwenye janga hili la mazingira:UN 

2 Juni 2022

Mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira ya binadamu, Stockholm+50, umeanza leo kwenye mji mkuu wa Sweden, Stockholm kwa wito kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizitaka nchi zote duniani kukumbatia haki za binadamu kwa ajili ya mazingira safi na yenye afya kwa wote hususan kwa jamii masikini, wanawake na wasichana, watu wa asili, vijana na vizazi vijavyo.  

 

Viongozi 7 vijana wameungana na Peace Boat huko Stockholm Sweden kuzindua awamu ya pili ya programu ya mabalozi vijana wa bahari na tabianchi.
Peace Boat-Ecoship
Viongozi 7 vijana wameungana na Peace Boat huko Stockholm Sweden kuzindua awamu ya pili ya programu ya mabalozi vijana wa bahari na tabianchi.

Mkutano huo ambao kwa mara ya kwanza ulifanyika Stockholm tarehe 5 mwezi Juni mwaka 1972 na kutoka na Azimio la Stockholm kuhusu maendeleo ya binadamu na mazingira umewaleta pamoja wadau zaidi ya 1000 kutoka nchi zaidi ya 100 duniani na wamezindua mpango wa hatua wa kuchagiza masuala ya kidijitali katika kusongesha maendeleo endelevu ya kimazingira na kijamii. 

Majanga matatu ya kihistoria 

Guterres amesema “dunia hivi sasa inakabiliwa na majanga matatu ya kihistoria , janga la mabadiliko ya tabianchi ambalo linakatili maisha ya watun na kutawanya wengine mamilioni kila mwaka." 

Janga linigne ni kumomonyoka kwa mfumo wa ikolojia ambao unachangia kupotea kwa bayoanuai na kuhatarisha maisha ya zaidi ya watu bilioni 3. 

Na janga la mwisho ni ongezeko la kiwango cha uchafuzi na taka ambalo linagharimu maisha ya takriban watu milioni 9 kila mwaka. 

 

Hali ya joto humaanisha kuyeyuka kwa barafu ya bahari, kuongezeka kwa halijoto ya bahari, na maji yenye joto - kuathiri mifumo ikolojia na mifumo ya hali ya hewa duniani.
WMO/Hwang Seonyoung
Hali ya joto humaanisha kuyeyuka kwa barafu ya bahari, kuongezeka kwa halijoto ya bahari, na maji yenye joto - kuathiri mifumo ikolojia na mifumo ya hali ya hewa duniani.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa “ustawi wa dunia uko katika hatari kubwa na kwa kiasi kikubwa ni kwa sababu hatujatimiza ahadi zetu kuhusu mazingira. Ingawa kumekuwa na mafanikio katika kuilinda sayari hii tangu mwaka 1972 ikiwemo kuokoa tabaka la ozone, lakini mifumo ya kiasilim ya dunia haiwezi kumudu matakwa yetu.” 

Tahadhari ya pato la taifa (GDP) 

Sehemu ya suluhisho iko katika kutoa pato la taifa (GDP) kama kipimo cha uwezo wa kiuchumi wa nchi, Katibu Mkuu ameendelea kusema , akiuelezea kama mfumo wa uhasibu "unaotunuku uchafuzi wa mazingira na taka". 

Ameongeza kuwa “tusisahau kwamba tunapoharibu msitu tunatengeneza pato la Taifa. Tunapovua samaki kupita kiasi, tunatengeneza pato la taifa .Pato la taifa si njia ya kupima utajiri katika hali ya sasa duniani.” 

Baada ya kutoa wito kwa mataifa yote kujitolea zaidi kutekeleza Malengo 17 ya maendeleo endelevu na kufuatia mkataba wa Paris wa 2015 ili kukabiliana na matishio hayo, Katibu Mkuu pia alisisitiza kuwa juhudi kubwa zaidi zinahitajika ili kufikia lengo la kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050. 

Ukame mkali unaua mifugo katika jamii ya wafugaji Higlo Kebele nchini Ethiopia.
© WFP/Michael Tewelde
Ukame mkali unaua mifugo katika jamii ya wafugaji Higlo Kebele nchini Ethiopia.

Joto kali 

"Hewa ya joto inatuua," amesema Katibu Mkuu , akirudia wito wake kwa nchi zote kuacha ruzuku ya mafuta kisukuku na kuwekeza katika nishati mbadala, wakati mataifa yaliyoendelea yanapaswa kutoa msaada wao "angalau mara mbili kwa kwa nchi maskini ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya majanga ya hali ya hewa.” 

Akisisitiza kwamba mataifa tayari yameshirikiana kulinda sayari katika nyanja nyingi, Bwna. Guterres amebainisha kwamba mabadiliko ya mwisho yanatarajiwa kuongezwa katika mfumo mpya wa kimataifa wa viumbe hai ili kurudisha nyuma upotevu wa bayoanuai ifikapo mwaka 2030. 

Kazi pia inaendelea ya kuanzisha mkataba wa kukabiliana na uchafuzi wa taka za plastiki, amesisitiza mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa bahari wa 2022 huko Lisbon,nchini Ureno, unatarajiwa kuchochea jitihada za kuokoa bahari yetu. 

"Ikiwa tutafanya mambo haya tunaweza kuepusha janga la hali ya hewa, kumaliza mzozo unaokua wa kibinadamu na usawa na kukuza maendeleo jumuishi na endelevu. Kila serikali, biashara na mtu binafsi ana jukumu la kutekeleza". 

(PHOTO) 

Msukumo wa kiteknolojia kwa uendelevu 

Katika maendeleo mengine yanayohusiana na hayo huko Stockholm leo  muungano unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wa wadau 1,000 kutoka zaidi ya nchi 100, wamezindua azma yao ya kutumia zana za kidijitali ili kuharakisha maendeleo endelevu ya kimazingira na kijamii. 

Muungano huo wa Uendelevu wa Mazingira kidijitali (CODES) utatoa njia za kujumuisha  uendelevu katika nyanja zote za masuala ya kidijitali.  

Hii ni pamoja na kujenga michakato inayojumuisha kimataifa ili kufafanua viwango na mifumo ya utawala kwa ajili ya uendelevu wa kidijitali, ugawaji wa rasilimali na miundombinu, huku pia ikibainisha fursa za kupunguza madhara au hatari zinazoweza kutokea kutokana na mfumo wa kidijitali, limesema shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter