Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa miaka 12 ya vita njaa imefurutu ada Syria, hatua zahitajika haraka: WFP

Familia iliyokimbia makazi yao ya kijiji cha El Teh, ambayo sasa inaishi katika kambi ya El Teh kaskazini magharibi mwa Syria.
© OCHA/Bilal Al-hammoud
Familia iliyokimbia makazi yao ya kijiji cha El Teh, ambayo sasa inaishi katika kambi ya El Teh kaskazini magharibi mwa Syria.

Kwa miaka 12 ya vita njaa imefurutu ada Syria, hatua zahitajika haraka: WFP

Msaada wa Kibinadamu

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP amehitimisha ziara yake nchini Syria na kutoa ombi kwa dunia kuwekeza kwa watu wa Syria na jamii zao ili kuwawezesha kujikimu kimaisha na kuacha kutegemea msaada wa chakula.

David Beasley amesema leo hii kufuatia miaka 12 ya vita, mdororo wa uchumi uliochangiwa na mfumuko wa bei, kuporomoka kwa sarafu ya taifa hilo na kupanda kwa bei ya chakula, watu milioni 12 hawajui mlo wao utakaofuata utatoka wapi .

Ameongeza kuwa watu wengine milioni 12 wako katika hatari ya kutumbukia kwenye janga la njaa ikimaanisha kuwa asilimia 70% ya watu wote hivi karibuni watashindwa kuweka mlo mezani kwa ajili ya famialia zao.

“Endapo tutashindwa kushughulikia mgogoro huu wa kibinadamu Syria mambo yatakuwamabaya zaidi ya tunavyofikiria. Je wimbi kubwa la watu kuhamia Ulya akama ilivyokuwa mwaka 2015 ndicho jumuiya ya kimataifa inachokitaka? Kama sivyo basi ni lazima tutumie fursa hii haraka kuepusha zahma kubwa inayojongea na kufanyakazi Pamoja kurejesha amani na utulivu kwa watu wa Syria.”

Familia inayoishi kwenye makazi yasiyo rasmi kwenye mji wa Raqqa, Kaskazini mwa Syria.
© UNICEF/Delil Souleiman
Familia inayoishi kwenye makazi yasiyo rasmi kwenye mji wa Raqqa, Kaskazini mwa Syria.

Beasley amezuru sehemu mbalimbali

Beasley, ambaye amezuru Syria mara tano hapo awali, alikwenda katika kitongoji cha Al Nashabiyah Duma huko Ghouta Mashariki mwa Damascus Vijijini.

Ghouta Mashariki ilijulikana kama kikapu cha mkate cha Damascus, na pia kwa bustani zake za matunda na mazao ya ubora wa mauzo ya nje.

Eneo hilo lilishambuliwa kwa kiasi kikubwa kati ya mwaka 2013 na 2018 na wakaazi wake walilazimika kuyahama makazi yao.

Katika kipindi hiki, WFP iliweza tu kufika eneo hilo kupitia misafara mitatu ya mashirika ya kibinadamu.

Tangu wakati huo, WFP imeanza kuwasaidia wakulima na jamii kwa kurekebisha baadhi ya mifereji ya umwagiliaji iliyoharibiwa wakati wa vita ili kuwasaidia kulima ngano na vyakula vingine ili waweze kujilisha wao na familia zao.

"WFP inafanya kazi kuwezesha kumwagilia karibu ekari 28,000 za ardhi nchini kote, kutosha kulisha watu 620,000 nchini humu. Hiyo inamaanisha njaa kidogo, fursa zaidi za kiuchumi, na uchumi imara wa ndani. Uwekezaji wa dola za milioni 14 utaokoa dola za Marekani milioni 50 kwa mwaka katika usaidizi wa kibinadamu, na kuunda karibu nafasi za ajira 90,000 katika taifa ambalo karibu asilimia 85% ya matumizi ya WFP yanakwenda kwa msaada wa chakula cha kibinadamu, hiyo ni akiba kubwa. Lakini tunahitaji kuongeza uwekezaji huu ili kuongeza mnepo wa jamii zingine zisizo na uhakika wa chakula kote Syria.” amesema Beasley.

Mama mkulima akipanda mbegu za mimea katika shamba ndogo Akkar, kaskazini mwa Lebanon.
UNDP Lebanon/Dalia Khamissy
Mama mkulima akipanda mbegu za mimea katika shamba ndogo Akkar, kaskazini mwa Lebanon.

Wakulima wanena yaliyo moyoni mwao

Beasley amep[ata fursa pia ya kusikia kutoka kwa wakulima ambao wameanza kulima chakula baada ya WFP kusaidia kurejesha mifumo ya umwagiliaji. Wamemwomba msaada wa kupata maji zaidi ili waweze kuanza tena kazi ya kilimo katika eneo hilo na kuzalisha chakula kwa vijiji vyao na maeneo ya jirani.

Bei za vyakula zimeongezeka karibu mara kumi na mbili katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Syria sasa inashika nafasi ya sita kwa idadi kubwa ya watu wasio na chakula duniani, ikiwa na watu milioni 2.5 ambao wana uhaba mkubwa wa chakula, na maisha yao yako hatarini bila msaada wa chakula.

Utapiamlo wa watoto na wajawazito unaongezeka kwa kasi ambayo haijawahi kuonekana  hata katika zaidi ya muongo mmoja wa vita.

WFP inatoa msaada wa kila mwezi kwa karibu watu milioni saba. Hii ni pamoja na mgao wa chakula, kuzuia na kutibu utapiamlo uliokithiri, milo ya shuleni, uhamishaji wa fedha taslimu na usaidizi wa kupata riziki, kuwajengea mnepo na usalama wa kijamii.

Ukarimu wa wafadhili umekuwa ufunguo wa kutoa msaada wa chakula cha kuokoa maisha kwa mamilioni ya watu ambao maisha yao yamesambaratishwa na zaidi ya muongo mmoja wa migogoro na kuyahama makazi yao.