Mabalozi wema wa IFAD wazindua ombi la dola milioni 200 kuzisaidia jamii za vijijini dhidi ya COVID-19

20 Aprili 2020

Mabalozi wema wa mfuko wa kimataifa wa maendeleo  ya kilimo IFAD leo wamezindua ombi la dola milioni 200 ili kuzisaidia jamii za vijiji kukabiliana na mlipuko wa janga la virusi vya Corona au COVID-19

Mabalozi hao mwigizaji, mtayarishaji filamu na mwanaharakati wa masuala ya kibinadamu Idris Elba na mcheza filamu, mlimbwende na mwanaharakati Sabrina Dhowre Elba wamezindua ombi hilo kupitia mfuko mpya wa kimataifa kwa ajili ya kupambana na Corona kwa niaba ya IFAD ili kuzuia athari za kiuchumi zinazosababishwa na COVID-19 zisisababishe janga la kimataifa la nja na mgogoro wa chakula.

Ukiwa tayari na dola milioni 40 kutoka kwa IFAF mfuko huo mpya “COVID-19 Rural Poor Stimulus Facility” unalenga kuchangisha angalau dola zingine milioni 200 kutoka kwa serikali, wakfu mbalimbali na sekta binafsi ili kupunguza athari za COVID-19 kwa wakulima wadogo wadogo na wazalishaji vijijini .

Akizungumzia uzinduzi wa mfuko huo Girlbert F. Houngbo Rais wa IFAD amesema “Nchi zinazoendelea tayari ziko hatarini na janga hili kama dharura ya kiafya na tusipochukua hatua sasa na haraka janga hili litakuwa mgogoro mkubwa wa chakula na njaa. Tunahitaji kuwekeza kwao na kuhakikisha mifumo ya chakula inaendelea kufanyakazi.”

Mwigizaji nyota wa Uingereza Idris Elba (Kushoto) na mkewe Sabrina Elba walipozuru Sierra Leone na mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD
© IFAD/Rodney Quarcoo
Mwigizaji nyota wa Uingereza Idris Elba (Kushoto) na mkewe Sabrina Elba walipozuru Sierra Leone na mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD

 

Kwa upande wake balozi mwema Sabrina Dhowre Elba amesema “Janga hilo limedhihirisha kwamba tuko salama tu kama wale wasiojiweza wako salama. Ni kwa faida yetu sote kuhakikisha mifumo ya chakula inaendelea, kuzilinda jamii za vijijini na kukabili janga hili la kiafya wakati watu waliopoteza ajira mijini wakirejea vijijini.”

Naye Idris Elba amesema “ Nchi zilizoendelea kiuchumi ziko katikati ya janga hili hivi sasa na bila shaka ni lazima zifanye kila ziwezavyo kusaidia watu wao. IFAD inahitaji msaada kuendelea na kazi ambayo inahitajika kuhakikisha mifumo ya chakula vijijini inaendelea kufanyakazi, endapo tunataka kuondoka kwenye janga hili na kuepuka madhila na njaa.”

IFAD inasema asilimia 80 ya watu wote masikini duniani wanaishi vijijini.

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter