Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asafiri kutoka Venezuela hadi Chile kwa mguu akiwa mjamzito, sasa anaona nuru

Andrelis Alvarez akiwa amembeba mwanae aliyejifungua njiani akiwa safarini kutoka Venezuela kuelekea Chile kusaka maisha bora. Hapa yuko Colchane nchini Chile kituo cha UNICEF cha kuhudumia familia za wahamiaji.
© UNICEF/Vera-Lisperguer
Andrelis Alvarez akiwa amembeba mwanae aliyejifungua njiani akiwa safarini kutoka Venezuela kuelekea Chile kusaka maisha bora. Hapa yuko Colchane nchini Chile kituo cha UNICEF cha kuhudumia familia za wahamiaji.

Asafiri kutoka Venezuela hadi Chile kwa mguu akiwa mjamzito, sasa anaona nuru

Wahamiaji na Wakimbizi

Huko Amerika ya Kusini Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake unaendelea kusaidia wahamiaji wanaokimbia ghasia na changamoto kwenye nchi zao.

Miongoni mwa walionufaika na msaada huo kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ni Andrelis Alvarez ambaye alivuka jangwa la Atacama na milima ya Andes akitokea Venezuela kuelekea Chile akiambatana na mpenzi wake, mtoto lakini zaidi akiwa na ujauzito.

Safari ilikuwa mbaya mno. Sitamani yeyote apitie nilichopitia!” anasema Andrelis akiwa Colchane, nchini Chile  mpakani na Bolivia, eneo lililo mita 3,800 kutoka usawa wa bahari, na baridi ni kali nyakati za usiku. Ni kwenye makazi ya wahamiaji.

Akikumbuka mapito ya safari na wale waliowasafirisha, Andrelis anasema, “kwenye safari yetu kutoka Venezuela kuelekea Ecuador walipora fedha zetu. Wasafirishaji walituahidi kuambatana nasi hadi mwisho wa safari, lakini walituacha nusu ya safari. Tulipita kwenye madimbwi makubwa, maji yalitufika hadi kifuani. Tulihofia kuwa mawakala wa uhamiaji wataturudisha nyumbani.”

Andrelis alihimili safari yote akiwa na ujauzito, sambamba na mtoto wake mwenye umri wa miaka minne na mpenzi wake. Wakiwa Lima, mji mkuu wa Peru, ndipo Andrelis alijifungua mtoto wa kiume na baada ya kujifungua anasema, “mtoto wangu alilazwa kwa siku 24 baada ya kuzaliwa kwa sababu ya baridi kali.”

Andrelis Alvarez (kulia) akiwa na mpenzi wake pamoja na watoto wao kwenye kituo cha familia za wahamiaji kinachoendeshwa na UNICEF mjini Colchane nchini Chile.
© UNICEF/Vera-Lisperguer
Andrelis Alvarez (kulia) akiwa na mpenzi wake pamoja na watoto wao kwenye kituo cha familia za wahamiaji kinachoendeshwa na UNICEF mjini Colchane nchini Chile.

Baadaye safari iliendelea kwa mguu na wakaweza kuvuka mpaka wa Bolivia na kuingia Chile ambako waliwasili katika kituo cha mpito cha mpakani Colchane kinachopatiwa usaidizi kutoka UNICEF.

Katika kituo hiki, mtoto mkubwa wa Andrelis alipatiwa matibabu dhidi ya kuhara, ugonjwa ambao ulimsubua safari nzima.

Glayson Dos Santos ni Naibu Mwakilishi wa UNICEF nchini Chile na anasema, “takribani watoto 40 wanapata huduma hapa. Iwapo tunamuona mtoto mwenye tatizo la afya, lishe au utapiamlo, basi tunampatia huduma ya awali.”

UNICEF kwa kushirikiana na wadau pamoja na serikali ya Chile wanahakikisha familia za wahamiaji zinakuwa salama na zinapata huduma ya elimu, afya, maji na ya kujisafi.

Na kwa Andrelis, hakuficha sababu ya wao kuvumilia safari ndefu ya milima na mabonde akisema, “lengo letu ni watoto wetu wawe bora na waishi kwenye mazingira tulivu. Ningependa kuona wanakuwa bora, na wanapata elimu nzuri. Mimi sikupata hiyo fursa lakini nataka wanangu wawe na fursa hii.”