Wavenezuela wazidi kukimbia nchi yao licha ya shida na taabu njiani

30 Agosti 2019

Wakati hali ya kisiasa na kiuchumi nchini Venezuela inazidi kuzorota raia zaidi wa Venezuela wanakimbilia mataifa mengine ya Amerika ya Kusini ambapo takriban raia milioni 4 wa Venezuala wameihama nchi yao. Kando na kuwepo hali mbaya ya usalama na ghasia pia kumeshuhudiwa ukosefu wa madawa, chakula na miundo msingi. 

Miongoni mwa raia hao wanaokimbia Venezuela ni Fabiana, mumewe na binti yao ambao waliishi katika jimbo la Miranda, kaskazini mwa Venezula.

Baada ya kupata habari kuhusu hitaji jipya la viza ya kuingia Peru kuanzia Juni 15, waliamua kuihama nchi yao kujiunga na dada yake Fabiana huko Santiago de Chile.

Walifunga safari ya siku kumi ya umbali wa kilomita 7,300 kuvuka bara la Amerika ya Kusini, kuanzia kaskazini kwenda kusini wakipitia Colombia, Ecuador na Peru wakilenga kufika Chile.

Wakipata makao kwenye kituo cha mabasi, hii imekuwa nyumbani kwa familia ya Fabiana kwa muda wa siku mbili.

Wameanzia Safari Venezuela wakipitia Colombia, Equador na sasa Peru.

Wakiwa na nia ya kupata makao salama huku wakiwakumbuka wale waliowaacha nyuma.

(sauti ya Fabiana Bernel)

“Familia yetu mara kwa mara hutuma ujumbe na kila wakati tunawajulisha tuko salama. Hatutaki kuwapa msongo wa mawazo. Katu sikuwahi kudhani kuwa nitakimbia nchi yangu.”

Raia milioni 4 wa Venezuela wameihama nchiwakikimbia ukosefu wa usalama, ghasia na hali ngumu ya maisha.

Wengi wamepewa makazi katika nchi ambazo zina changamoto za kujikimu. Fabiana aliuza mali yao yote kugharamia safari.

Chile imekuwa kituo kikuu kwa wakimbizi kutoka Venezuela na pia kwa wahamiaji. Lakini wengi hawafanikiwa kuvuka na wao hulala kwenye mpaka kwenye kibaridi. Federico Luis Agustin ni mwakilishi wa UNHCR nchini Peru.

(Sauti ya Federico Luis Agusti)

 “Baadhi ya watu hawana nyaraka zinazohitajika kuingia Chile. Baadhi wamepoteza vitambulisho vyao, hati za kusafiria, wakiwa njiani au waliporwa. Wengine hawana nyaraka za kuthibitisha kibali cha malezi ya watoto. Vyote hivi vinatahiji mchakato mpakani na hii inazuia watu kuingia kwa njia ya kawaida.”

 Familia ya Fabiana ilirudishwa wakati walijaribu mara ya kwanza, lakini wameshikilia malengo yao kipindi hiki.

(Sauti ya Fabiana Bernel)

“Iwapo utaweka lengo lako lazima ulifikie. Bila shaka bila kumweka mtu yeyote hatarini, hasa binti yangu. Hicho ndicho nataka kuepuka, sitaki kumweka binti yangu hatarini na ndio maana nimemwondoa hapa.”

Wakati wa jaribio la pili, Fabiana , mumewe na binti yao walivuka. Kwa sasa wama matumaini kuwa watakuwa na bahati nzuri kufika Chile na kuwa karibuni watajumuika tena na familia yao.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud