Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuungane kupambana na mashambulizi dhidi ya wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela.

Familia hii ya wavenezuela ilipowasili nchini Peru, ilipokelewa kwa ukarimu mkubwa. Hivi sasa wanaishi kwa amani na familia hiyo imewapatia chumba kidogo cha kuishi.
UNHCR/Elisabet Diaz Sanmartin
Familia hii ya wavenezuela ilipowasili nchini Peru, ilipokelewa kwa ukarimu mkubwa. Hivi sasa wanaishi kwa amani na familia hiyo imewapatia chumba kidogo cha kuishi.

Tuungane kupambana na mashambulizi dhidi ya wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela.

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lile la uhamiaji IOM hii leo wametoa taarifa ya pamoja mjini Geneva Uswisi wakizitaka nchi za Amerika ya kusini kukemea kwa pamoja mashambulizi na lugha ya chuki dhidi ya wavenezuela wanaosaka hifadhi katika nchi  jirani na nchi yao.

Eduardo Stein mwakilishi maalumu wa UNHCR na IOM kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela ametoa maoni yake baada ya mwishoni mwa wiki Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili kuhusu hali ya Venezuela ambako kiongozi wa upinzani Juan Guaidó alijitangaza kuwa rais wa nchi hiyo tarehe 23 mwezi huu wa Januari 2018.

Kufuatia tahadhari kuwa mapokezi ya wavenezuela katika nchi za jirani yalikuwa si ya kufurahisha Stein ambaye ni makamu wa rais wa zamani wa Guatemala amezisihi nchini kadhaa ambazo hakuzitaja akisema, “vitendo hivi vya chuki, kutokuvumiliana na ubaguzi vinaleta wasaiwasi mkubwa. Ubaguzi wa rangi, jinsia na utaifa havina nafasi katika nchi zetu na vinapaswa kukemewa.”

Wakati akiwasihi viongozi wa kisiasa na wadau wengine kuhamasisha amani, haki, utulivu na usitahimilivu, bwana Stein ameeleza umuhimu na wajibu wa vyombo vya habari vya asili na vya kisasa vya mitandaoni kusaidia katika suala hili.

Watu 233 kutoka Venezuela waondoka Boa Vista katika awamu ya pili ya utaratibu wa kuwahamisha ambapo waomba hifadhi kutoka Venezuela wanawasili katika miji karibu na mipaka wanoahmishwa maeneo mengine ya Brazil. Aprili 5, 2018
© UNHCR/Luiz Fernando Godinho
Watu 233 kutoka Venezuela waondoka Boa Vista katika awamu ya pili ya utaratibu wa kuwahamisha ambapo waomba hifadhi kutoka Venezuela wanawasili katika miji karibu na mipaka wanoahmishwa maeneo mengine ya Brazil. Aprili 5, 2018

 “Vyombo vya habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii wanapaswa kuripoti ukweli katika namna ya kuwajibika bila kupandikiza ubaguzi na wanatakiwa kulaani mashambulizi yoyote yawe ya mwili au kwa maneno dhidi ya wakimbizi au wahamiaji”

Kwa mujibu wa UNHCR na IOM, maelfu ya watu wanaendelea kuikimbia Venezuela kila siku kufuatia janga la kibinadamu linaloendelea likihusishwa na anguko la uchumi na mgogoro wa kisiasa unaoendelea.

Zaidi ya wavenezuela milioni tatu wameikimbia nchi yao tangu mwaka 2015, watu milioni 2.4 wakikimbilia katika nchi za jirani wengi wao takribani milioni moja wakiwa nchini Colombia na wengine wakiwa 500,000 nchni Peru, zaidi ya 220,000 wakiwa Ecuador, Argentina ikiwa na watu 130,000 zaidi ya 100,000 wakiwa Chile na Brazil 85,000.