Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkwamo wa barabara haukuzuia vifaa vya shule kufikia wanafunzi

Maeneo ambako magari hayawezi kufika, baiskeli zinatumika kufikisha vifaa vya shule kwenye majimbo 6 yaliyonufaika na mradi wa Kurejea Shuleni.
UNICEF Burundi
Maeneo ambako magari hayawezi kufika, baiskeli zinatumika kufikisha vifaa vya shule kwenye majimbo 6 yaliyonufaika na mradi wa Kurejea Shuleni.

Mkwamo wa barabara haukuzuia vifaa vya shule kufikia wanafunzi

Utamaduni na Elimu

Tarehe 24  mwezi  huu wa Januari ni siku ya elimu duniani ikimulika mafanikio na changamoto za kufanikisha lengo namba 4 la kufanikisha elimu bora kwa kila mtu kokote aliko. Elimu bora ni pamoja na vifaa vya ikiwemo madaftari, vitabu na kalamu ambako kwa watoto wengine bado vinasalia kuwa anasa.

Mathalani nchini Burundi ambako huko katika baadhi ya maeneo wazazi wanalazimika kufanya vibarua wao na watoto wao ili waweze kumudu madaftari ya shuleni. Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake na wadau wamebaini changomoto hiyo na kusambaza vifaa kwenye majimbo sita ya taifa hilo la Maziwa Makuu barani Afrika. 

Lea Tuyisenge akifurahia baada ya kupokea vifaa vya shule kutoka UNICEF na wadau.
UNICEF Burundi
Lea Tuyisenge akifurahia baada ya kupokea vifaa vya shule kutoka UNICEF na wadau.

Wazazi walikuwa na hofu na hata kufanya vibarua na watoto wao

Baadhi ya wazazi kama vile Renate Mukarutamo mama wa watoto sita mkazi wa kijiji cha Mishiha, jimboni Cankuzo, walikuwa na hofu kubwa.

Bi, Mukarutano anasema hakufahamu ni vipi anaweza kununua vifaa vya shule kwa watoto wake wote sita, kwani gharama imepanda kutoka dola senti 80 hadi zaidi ya dola moja kulingana na idadi ya makaratasi kwenye daftari. 

Anasema hofu yake kubwa ilikuwa ni uwezo wa kununua daftari lenye makaratasi zaidi ya 100.  

UNICEF na wadau walibaini changamoto hiyo

UNICEF ilitambua changamoto ya Renata na wazazi wengine na hivyo kupitia kampeni yake ya wanafunzi kurejea shule kwa mwaka wa shule 2022-2023 ilisambaza vifaa vya shule kwenye majimbo sita ya Cankuzo, Kirundo, Makamba, Muyinga, Rumonge na Ruyigi. 

Kampeni inaendeshwa na UNICEF kwa ushirikiano na wadau ambao ni Ubia wa Kimataifa wa Elimu duniani, GPE na Benki ya Dunia. 

Vifaa vilipakiwa kwenye malori na kupita vilima na mabonde kufikia kila eneo na ambako barabara ilikuwa haipitiki, baiskeli zilitumika.  

Hemedi Kirosho ni msafirishaji mizigo kwa malori jimboni Cankuzo mashariki mwa Burundi anasema, “kuna shule ziko maeneo ambayo barabara hazipitiki. Kama barabara ina utelezi tunatumia baiskeli.” 

Sylvere Ntihoro, Mkurugenzi wa elimu ya msingi wilaya ya Kigamba jimboni Cankuzo anazungumzia changamoto za kutokuwa na vifaa vya shule, halikadhalika kwa wazazi akisema, “kama mtoto hana vifaa vya kutosha vya shule, inakuwa vigumu sana kujifunza. Kwa msaada huu wa vifaa, wazazi hawatokuwa na mkwamo wa kupeleka watoto wao shuleni. Halikadhalika, walimu watafarijika zaidi.”

Soundcloud

Watoto wa wazazi watoa shukrani

Vifaa vimewasili na watoto jimboni Cankuzo wako darasani na wamepatiwa vifaa ikiwemo vitabu na madafari na kalamu, miongoni mwao ni mtoto wa kiume wa Bi. Mukarutamo aitwae Lea na akitabasamu anasema, “sasa nina vifaa vyote vya shule  hivyo nitaendelea na masomo hadi niwe daktari na hatimaye nitibu watu.” 

Kisha ni safari kurejea nyumbani akiwa na vifaa vyake, na mama yake mzazi anafunguka akisema, “nilikuwa nina hofu kubwa. Sasa hii kampeni ya Kurejea shuleni inawapatia vifaa vya shule. Nilikuwa nina madaftari machache nikahofia nitawapatiaje wote ikizingatiwa kuwa wakati wa likizo mimi na watoto wangu ilibidi tufanye vibarua kwa watu ili tuweze kununua vifaa hivyo. Ninawashukuru wote waliotusaidia.” 

Mwaka huu wa shule wa 2022-2023 zaidi ya watoto milioni moja katika majimbo hayo sita wamepatiwa vifaa vya shule.