Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2023 waanza kwa joto, katikati ya msimu wa baridi Ulaya yafikia joto la msimu wa kiangazi 

Kuchomoza kwa jua katika Delta ya Ebro katika eneo la Catalonia nchini Hispania..
WMO/Agusti Descarrega Sola
Kuchomoza kwa jua katika Delta ya Ebro katika eneo la Catalonia nchini Hispania..

Mwaka 2023 waanza kwa joto, katikati ya msimu wa baridi Ulaya yafikia joto la msimu wa kiangazi 

Tabianchi na mazingira

Mamia ya vituo vya hali ya hewa kote Ulaya vimerekodi viwango vya juu vya joto zaidi kila siku kuwahi kufikiwa katika miezi ya Desemba au Januari. Huduma kadhaa za kitaifa za hali ya hewa na maji kutoka bara hilo zinathibitisha kuwa mwaka wa 2022 ulikuwa wa joto zaidi katika historia katika nchi zao, shirika la umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa duniani (WMO) limeripoti leo Alhamisi.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesisitiza kuwa halijoto iliyozidi nyuzijoto 20 za selisiasi ilitokea katika nchi nyingi za bara hilo hata Ulaya ya Kati na kwamba katika mataifa kadhaa, kutoka Uhispania hadi Ulaya Mashariki, rekodi zingine za halijoto ya kitaifa zilivunjwa na maeneo mengi katika miezi ya Desemba na Januari.


Mamia ya vituo vya hali ya hewa kote Ulaya vilirekodi halijoto ya juu zaidi ya kila siku kuwahi kufikiwa katika miezi hiyo miwili. Kwa mfano, mnamo Desemba 31, zebaki ilifikia rekodi ya juu ya 25.1°C katika jiji la Bilbao nchini Hispania, na kuzidi 24.4°C mnamo Januari 1, 2022.


Mifano mingine mizuri zaidi ya halijoto ya juu katika siku ya mwisho ya mwaka 2022 ilikuwa nyuzijoto 18.9°C iliyofikiwa katika Warsaw, mji mkuu wa Poland, ambayo ilizipita nyuzijoto 13.8°C ya Januari mwaka 1993; au nuzijoto 19.4°C iliyorekodiwa katika jiji la Ujerumani la Dresden, ambalo lilipunguza joto la juu kabisa la 17.7°C mnamo Desemba 5, 1961.


“Eneo la mgandamizo wa juu wa bonde la Mediterania na mfumo wa Atlantiki wa mgandamizo wa chini lilisababisha mtiririko mkali wa kusini-magharibi ambao ulileta hewa ya joto kutoka kaskazini-magharibi mwa Afrika hadi latitudi za kati. Katika mashariki ya Atlantiki ya Kaskazini, halijoto ya uso wa bahari ilikuwa kati ya 1 na 2°C juu kuliko kawaida, na karibu na ufuo wa Peninsula ya Iberia ongezeko hili lilikuwa kubwa zaidi.”  Inasema taarifa ya WMO.


Kuchapishwa kwa rekodi hizi za juu kumeendana na uthibitisho wa vituo kadhaa vya kitaifa vya hali ya hewa na kihaidrolojia vya Ulaya -kama vile AEMET (Hispania), Meteo France (Ufaransa), Deutscher Wetterdienst (Ujerumani) na Met Office (Uingereza)- kwamba mwaka wa 2022 ulikuwa. joto zaidi katika historia katika nchi zao.


Data za hivi karibuni za WMO zinazohusiana na Ulaya


Mzunguko na ukubwa wa matukio ya joto kali, ikiwa ni pamoja na mawimbi ya joto baharini, yameongezeka katika miongo ya hivi karibuni na inakadiriwa kuendelea kuongezeka bila kujali hali ya utoaji wa gesi chafuzi.


Viwango muhimu vya mifumo ikolojia na binadamu vinakadiriwa kupitwa na ongezeko la joto duniani la 2°C au zaidi juu ya viwango vya kabla ya viwanda kufikia mwisho wa karne hii. Mkataba wa Paris unaweka lengo la kupunguza ongezeko hili hadi kiwango cha juu cha nyuzijoto 1.5°C.


WMO ilichapisha Ripoti ya Hali ya Hali ya Hewa barani Ulaya mwaka 2021 miezi miwili iliyopita, ambapo iliripotiwa juu ya ongezeko kubwa la halijoto barani Ulaya katika kipindi cha mwaka 1991-2021, kwa wastani wa takriban +0.5°C kwa muongo mmoja, ya juu zaidi ya mabara yote ya dunia na ukuaji wa zaidi ya mara mbili ya wastani wa dunia.


WMO inasema licha ya hali ya La Niña kupunguza halijoto duniani kwa mwaka wa pili mfululizo, mwaka wa 2022 huenda ukabaki mwaka wa 5 au 6 kuwa na joto zaidi duniani.