Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuiya ya kimataifa na wadau wa mazingira wakaribisha Mfumo mpya wa Kimataifa wa Bayonuai (GBF)

CBD umepitisha makubaliano ya kihistoria yaliyofikiwa katika mkutano huo kuhusu mpango mpya wa kuhifadhi na kulinda asili kwa kutumia Mfumo mpya wa Kimataifa wa Bayonuai, (GBF).
Picha: UN Biodiversity
CBD umepitisha makubaliano ya kihistoria yaliyofikiwa katika mkutano huo kuhusu mpango mpya wa kuhifadhi na kulinda asili kwa kutumia Mfumo mpya wa Kimataifa wa Bayonuai, (GBF).

Jumuiya ya kimataifa na wadau wa mazingira wakaribisha Mfumo mpya wa Kimataifa wa Bayonuai (GBF)

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo ni tamati ya mkutano wa 15 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa kuhusu bayonuai, COP15, huko Montréal, Canada, wadau mbalimbali wa mazingira wamekaribisha makubaliano ya kihistoria yaliyofikiwa katika mkutano huo kuhusu mpango mpya wa kuhifadhi na kulinda asili kwa kutumia Mfumo mpya wa Kimataifa wa Bayonuai, (GBF).

Kupitia taarifa iliyotolewa Jumatatu hii ya leo tarehe 19 Desemba huko mjini Montreal, Canada ulikokuwa unafanyika mkutano huo wa COP 15, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP, Achim Steiner, ameeleza kuwa Makubaliano haya yaliyofikiwa yanamaanisha kuwa watu kote ulimwenguni wanaweza kuwa na matumaini ya maendeleo ya kweli katika kukomesha upotevu wa bayonuai na kulinda na kurejesha ardhi na bahari kwa njia ambayo inalinda sayari dunia na kuheshimu haki za watu wa asili na jumii za wenyeji. 

Kasuku hupatikana zaidi katika mabara ya kitropiki na mikoa mengine kote ulimwenguni.
Unsplash/Roberto Nickson
Kasuku hupatikana zaidi katika mabara ya kitropiki na mikoa mengine kote ulimwenguni.

Bwana Steiner amedokeza kuwa mambo yaliyoidhinishwa katika Mkutano huo wa 15 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa kuhusu bayonuai yanajumuisha shabaha nyingi muhimu ambazo zinasimamia hatua ambazo ni lazima zichukuliwe ili kukomesha upotevu wa bayonuai, jinsi ufadhili kuhusu jambo hili unavyofanywa na jinsi maendeleo yatakavyofuatiliwa na kuripotiwa. 

“Jumuiya ya kimataifa imekusanyika na kukubaliana kuhusu njia kabambe. Sasa, lazima tuendeleze maono haya.” Amesema Bwana Steiner akiongeza kwamba kwa upande wao kupitia ‘Ahadi ya Mazingira ya UNDP,’ pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa Mazingira, UNEP na wadau wengine, wamejitolea kugeuza mwongozo huu kutoka kwenye maneno kuwa ukweli na kwamba wako tayari kuchua hatua kwa vitendo.  

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa UNDP, sasa zaidi ya nchi 140 zitaungwa mkono kupitia mkakati wa ‘Ahadi ya Mazingira ya UNDP’ katika kuhakikisha bayonuai ya dunia inatunzwa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen amesema anakaribisha kupitishwa kwa Mfumo wa Kimataifa wa Bayonuai. Na kwamba “mafanikio yatapimwa na maendeleo yetu ya haraka na thabiti katika utekelezaji, yale ambayo tumekubaliana. Mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa unalenga kusaidia utekelezaji wake ili kweli tuweze kufanya amani na asili.”