Afrika Magharibi inaongoza kwa kupunguza watu wasio na utaifa barani Afrika-UNHCR

2 Machi 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limepongeza nchi wanacaham wa jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS kwa mafanikio ya kutaka kumaliza tatizo la kutokuwa na utaifa lakini pia likasihi juhudi kuongezwa maradufu ili kuhakikisha kila mtu katika ukanda huo anakuwa na utaifa na anafaidika na haki za uraia.

Taarifa iliyotolewa leo na UNHCR imesema tangu kupitishwa kwa azimio la Abidjan mnamo mwezi Februari mwaka 2015 na wanachama wote wa ECOWAS, nchi 12 kati ya 15 tayari zimeridhia  mikataba miwili ya Umoja wa Mataifa kuhusu watu wasio na utaifa. Nchi tisa za ECOWAS tayari zimeweka mipango ya kitaifa ya utekelezaji ili kutatua na kuzuia ukosefu wa utaifa.

Kwa msaada wa UNHCR na wadau wake, kampeni za uandikishaji wa vizazi zimefanywa katika nchi nne, Mali, Niger, Burkina Faso na Côte d’Ivoire. Mathalani nchini Côte d’Ivoire, usajili wa kuzaliwa kwa watoto wa umri wa kwenda shule umewanufaisha watoto 400,000 na hvyo kupunguza hatari ya kukosa utaifa na kuwasaidia kuwa na uhakika wa kupata elimu.

Kwa upande wa Sierra Leone imeondoa ubaguzi wa kijinsia katika sheria yake ya utaifa ambayo ilikuwa inawazuia akina mama kuwapatia uraia watoto wao kama ambavyo wanaume wangeweza kufanya. Liberia nayo imeahidi kufanya hivyo mwaka ujao.

Mkurugenzi wa UNHCR ofisi ya kanda ya Afrika Magharibi na kati, Millicent Mutuli amesema, “tunaona maendeleo makubwa katika marekebisho ya sera na sheria kushughulikia suala la ukosefu wa utaifa katika ukanda huu. Hili ni dhihirisho la kipekee la utashi wa kisiasa na kujitolea.”

Azimio la Abidjan ni mkakati wa ukanda huo wa Afika Magharibi kuendana na kampeni ya kimataifa ya UNHCR inayofahamika kama #IBelong yenye lengo la kutokomeza tatizo la ukosefu wa utaifa iliyozinduliwa mwaka 2014 kuzihamasisha serikali na wadau kutatua suala la ukosefu wau taifa ndani ya kipindi cha miaka kumi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud