Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ECW na wadau waleta nuru kwa watoto Ethiopia katikati ya janga la elimu

Watoto wakiimba wakati wa ziara ya pamoja ya ujumbe wa ECW na Norway kwenye maeneo yanayonufaika na miradi ya pande mbili hizo nchini Ethiopia
ECW
Watoto wakiimba wakati wa ziara ya pamoja ya ujumbe wa ECW na Norway kwenye maeneo yanayonufaika na miradi ya pande mbili hizo nchini Ethiopia

ECW na wadau waleta nuru kwa watoto Ethiopia katikati ya janga la elimu

Utamaduni na Elimu

Licha ya kwamba hatma ya elimu nchini Ethiopia iko mashakani wakati huu ambapo taifa hilo la Pembe ya Afrika likikabiliwa na janga baya zaidi la kibinadamu kuwa kukumbwa nalo katika miongo kadhaa, mfuko wa Umoja wa Mataifa wa elimu taratibu unaleta nuru kule ambako miradi yake imebisha hodi. 

Tathmini hiyo infuatia ziara ya pamoja nchini humo ya uongozi kutoka Education Cannot Wait, ECW, au kwa lugha ya Kiswahili Elimu Haiwezi Kusubiri, ambao ni mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kusongesha elimu duniani, ziara iliyomshirikisha pia Waziri wa Norway wa Maendeleo ya Kimataifa na wadau wengine wa kimataifa. 

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na ECW na Norway katika miji ya Addis Ababa, Ethiopia na New York, Marekani imesema ujumbe huo ulitathmini hatua na mahitaji ya elimu kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mizozo, mabadiliko ya tabianchi, utapiamlo na ukimbizi wa ndani. 

Mtoto wa kike akitabasamu darasani wakati wa ziara ya pamoja ya ECW na Norway nchini Ethiopia.
ECW
Mtoto wa kike akitabasamu darasani wakati wa ziara ya pamoja ya ECW na Norway nchini Ethiopia.

Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF zinaonesha kuwa idadi ya watoto wasio shuleni nchini Ethiopia kutokana na dharura hizo imeongezeka kutoka watoto milioni 3.1 hadi watoto milioni 3.6 katika kipindi cha miezi 6. 

Mapigano ya hivi karibuni kwenye majimbo ya Afar, Amhara na Tigray yamefurusha familia kutoka maeneo yao na ghasia zinazoendelea sasa kwenye maeneo ya Oromia zinasababisha ukimbizi zaidi. 

Kuna mabadiliko kule ambako miradi imefika 

Wakati wa ziara hiyo ya pamoja, Anne Beathe Tvinnereim, Waziri wa Norwaya wa Maendeleo ya kimataifa, Graham Lang, Mkurugenzi wa ECW akihusisha na mkutano wa ufadhili na wadau wengine walikutana na watoto na vijana barubaru walioathiriwa na majanga yanayoendelea kwenye majimbo ya Oromia na Somali. 

Walitembea shule na jamii zinazonufaika na miradi ya pamoja ya elimu inayofadhiliwa na ECW, UNICEF, Save the Children Ethiopia na wadau wengine kwa ushirikiano na serikali. 

Kupitia program za ECW na wadau, jamii imehamasika kwenye elimu, vyama vya walimu na wazazi vimeshamiri, vilabu vya wanafunzi halikadhalika, huku idadi ya watoto wanaoandikishwa na kumaliza masomo ikiongezeka hasa miongoni mwa wasichana. 

Nchini Ethiopia pekee, ECW imewekeza dola milioni 55 tangu mwaka 2017 pamoja na nyongeza ya uwekezaji wa dola milioni 5 inayokamilishwa ili kuchagiza elimu kwenye maeneo ya ukame. 

Mtoto akizungumza darasani wakati wa ziara ya pamoja ya ECW na Norway kwenye maeneo ambako pande mbili hizo zinatoa misaada nchini Ethiopia ili kuboresha elimu.
ECW
Mtoto akizungumza darasani wakati wa ziara ya pamoja ya ECW na Norway kwenye maeneo ambako pande mbili hizo zinatoa misaada nchini Ethiopia ili kuboresha elimu.

Idadi ya wanafunzi wanaohitimu masomo imeongezeka 

Kwa kipindi cha miaka mitatu, mradi mpana wa kusaidia elimu umefikia zaidi ya wasichana na wavulana 250,000 nchini Ethiopia, mradi unaohusisha mlo shuleni, usaidizi wa kisaikolojia, mafunzo kwa walimu, vifaa vya shule, mbinu za kuchochea ufundishaji na mafunzo, mipango ya mafunzo kuhusu jinsia na ujenzi na ukarabati wa majengo ya shuleni. 

“Inatia moyo sana kuona matokeo chanya ya mradi huu tunaotekeleza pamoja,  matokeo chanya kwa jamii na watoto,” amesema Bwana Lang, kutoka ECW huku akiongeza kuwa “kuanzia usawa wa jinsia, hadi kuhimili mabadiliko ya tabianchi, mbinu ambazo zimebuniwa kushughulikia mahitaji mahsusi kwa watoto walioathirika na majanga na pia kuboresha matokeo yao ya kujifunza.” 

Amesema ECW na wadau wanatoa wito kwa wafadhili wa umma na kutoka sekta binafsi kuongeza fedha kwa ECW ili waweze kupanua wigo wa program hiyo ili iwafikie watoto wengi zaidi. 

Bi. Beathe Tvinnereim amesema “utoaji wa elimu kwenye maeneo yenye mizozo ni kipaumbele cha serikali ya Norway. Kwenye mizozo, watoto wa kike na wasichana ndio wanakuwa watoro zaidi. Kile ambacho ziara hii mashinani imetufundisha ni kwamba iwapo unaweza kurejesha watoto shuleni, basi hatimaye wataweza kusaidia kujenga jamii yao wanamoishi.”