Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Historia ya utumwa bado ina makovu kwa jamii yanayodumaza maendeleo: Guterres

Watoto nchini Burkina Faso wanajihusisha na aina mbaya zaidi ya ajira kwa watoto, ikiwa ni pamoja na katika uchimbaji wa dhahabu bandia na uchimbaji wa dhahabu
© UNICEF/Christine Nesbitt
Watoto nchini Burkina Faso wanajihusisha na aina mbaya zaidi ya ajira kwa watoto, ikiwa ni pamoja na katika uchimbaji wa dhahabu bandia na uchimbaji wa dhahabu

Historia ya utumwa bado ina makovu kwa jamii yanayodumaza maendeleo: Guterres

Haki za binadamu

Historia au urithi ulioachwa na biashara ya utumwa katika bahari ya Atlantiki unaendelea hadi leo, kama vile utumwa wa kisasa unavyoongezeka, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres. 

Katika ujumbe wake kwa ajili ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya kukomesha utumwa, leo tarehe 2 Disemba, Bwana. Guterres amesema kwamba jamii zinaendelea kuathirika kutokana na mateso ya kihistoria ya Waafrika waliokuwa watumwa, na hauwezi kumpa kila mtu fursa sawa za maendeleo. 

Kutokomeza utumwa sasa 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia amehimiza hatua zichukuliwe kutambua na kujitolea tena kutokomeza aina zote za utumwa wa kisasa, kuanzia kwa watu wanaofanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu hadi kwa ukatili wa kingono, ajira kwa watoto, ndoa za shuruti na matumizi ya watoto katika vita vya silaha. 

Akinukuu makadirio ya hivi karibuni ya dunia kuhusu utumwa wa kisasa wa kazi za kulazimishwa na ndoa za shuruti Guterres amesema watu milioni 50 walifanywa watumwa katika kipindi cha mwaka jana uliopita. 

Alifafanua kuwa makundi yaliyotengwa ndiyo yaliyo hatarini zaidi, kama vile ya makabila, dini na lugha ndogo, pamoja na wahamiaji, watoto na watu kutoka makundi ya LGBTI na kwamba wengi wa watu hawa walio hatarini ni wanawake. 

Amesisitiza kwamba "Hatua za ziada zinapaswa kuchukuliwa kwa ushirikishwaji kamili wa wadau wote, ikiwa ni pamoja na sekta binafsi, vyama vya wafanyakazi, mashirika ya kiraia na taasisi za haki za binadamu. Pia natoa wito kwa nchi zote kulinda na kudumisha haki za waathiriwa na manusura wa utumwa." 

Utumwa unaongezeka 

Makadirio ya hivi karibuni ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani ILO, yanaonyesha kuwa kazi za kulazimishwa na ndoa za shuruti zimeongezeka sana katika miaka mitano iliyopita. 

Kulikuwa na takriban watu milioni 10 zaidi waliokuwa watumwa mwaka 2021, ikilinganishwa na makadirio ya kimataifa ya mwaka 2016, kulingana na Umoja wa Mataifa, na kuleta jumla ya watutu waliokuwa watumwa kufikia milioni 50 duniani kote. 

Ingawa utumwa wa kisasa haujafafanuliwa katika sheria, unatumika kama neno mwavuli linalojumuisha mazoea kama vile kazi za kulazimishwa, utumwa wa madeni, ndoa za shuruti na biashara haramu ya binadamu. 

Utumwa bado umeenea 

Utumwa unajumuisha hali zote za unyonyaji ambapo mtu hawezi kukataa, au kuondoka, kwa sababu ya vitisho, vurugu, kulazimishwa, udanganyifu, au matumizi mabaya ya mamlaka. 

Ujumbe wa Katibu mkuu unasema utumwa wa kisasa unatokea karibu kila nchi duniani, na unapita katika misingi ya kikabila, kitamaduni na kidini. 

Kinyume na dhana iliyozoeleka na kutawala, baadhi ya asilimia 52 ya kazi zote za kulazimishwa na robo ya ndoa zote za shuruti, zinaweza kupatikana katika nchi za kipato cha kati cha juu au za kipato cha juu. 

Takriban watu 4 kati ya 5 walio katika ukatili wa kijinsia wa kulazimishwa katika biashara ya ngono, ni wanawake au wasichana. 

Kitengo cha takwimu za kimataifa za kazi za kulazimishwa 

Sambamba na Siku ya Kimataifa, ILO inazindua kitengo kipya cha kuangalia kazi za Kulazimishwa (FLO), kilichoundwa na mradi wa Daraja wa ILO ili kujibu ombi la magavana wa shirika la ILO la “kuunda  kitengo cha takwimu za kimataifa  kuhusu kazi ya kulazimishwa na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu." 

Hifadhidata ya FLO itakuwa hifadhi ya taarifa za kimataifa na ngazi ya nchi kuhusu kazi ya kulazimishwa -"kitengo kimoja kwa ajili ya taarifa kuhusu janga hilo.” 

Wasifu wa nchi umetengenezwa kwa ajili ya nchi zote 187 wanachama wa ILO kwa kutumia taarifa zinazopatikana hadharani kutoka kwa vyanzo vinavyotambulika, ili kutoa muhtasari wa hatua za kitaifa za kukabiliana na uhalifu huu.