Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mwanamume akiwa na bango linalosema 'bado utumwa upo' akiwa Marekani.

Tujifunze kwa yaliyopita, tushikamane kutokomeza ubaguzi wa rangi:Guterres 

© Unsplash/Hermes Rivera
Mwanamume akiwa na bango linalosema 'bado utumwa upo' akiwa Marekani.

Tujifunze kwa yaliyopita, tushikamane kutokomeza ubaguzi wa rangi:Guterres 

Haki za binadamu

 Hii leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kumbukizi ya waathirika na manusura wa biashara ya utumwa katika bahari ya Atlantiki Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “kuna mengi tunayofahamu kuhusu biashara hiyo na leo ni siku ya kukumbuka uhalifu dhidi ya binadamu, usafirishaji na biashara haramu ya binadamu pamoja na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu usioweza hata kuzungumzika.”  

Katika ujumbe wake maalum wa siku hii amesema kama hiyo haitoshi watu wenye asili ya Afrika bado wanaendelea kubaguliwa kwa misingi ya rangi na kuenguliwa na hivyo ametaka kuungana ili kujenga jamii zenye misingi ya utu, usawa na mshikamano.  

Ameongeza kuwa kwa zaidi ya miaka 400, wanaume, wanawake na watoto milioni zaidi ya milioni 15 walikuwa waathiriwa wa biashara mbaya ya utumwa iliyovuka bahari ya Atlantiki, katika moja ya sura mbaya zaidi katika historia ya mwanadamu. 

"Kuna mengi tunayojua kuhusu biashara ya kuvuka Atlantiki kwa Waafrika waliofanywa watumwa,"  

Amesema huo ni uhalifu wa wazi dhidi ya ubinadamu, akiashiria kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha biashara haramu ya binadamu iliyofanyika, miamala duni ya kiuchumi inayohusika, na ukiukwaji usioelezeka wa haki za binadamu. 

Sera za ubaguzi wa rangi zinaendelea 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa "Pia kuna mengi ambayo hatujui, na leo ni siku ya kujifunza". 

Nyuma ya ukweli na takwimu, amekumbusha kwamba kuna mamilioni ya hadithi za kusikitisha za wanadamu. 

"Hadithi za mateso na maumivu yasiyoelezeka ya familia na jamii zilizosambaratika lakini pia hadithi za ujasiri wa kutisha na ukaidi dhidi ya ukatili wa wakandamizaji". 

Ingawa ulimwengu hautawahi kujua kila kitendo cha upinzani kikubwa au kidogo ambacho japo polepole lakini kwa hakika kilishinda udhalimu, ukandamizaji na utumwa, hadithi hizo ni muhimu kwa ufahamu wetu wa siku za nyuma ambazo ni za urithi mbaya zaidi na unaoendelea unaendelea kuighubika dunia yetu ya sasa: “ubaguzi wa rangi”. 

Mnyororo wa pingu uliotumika kufungia watumwa ukiwa sehemu ya maonesho kuhusu biashara ya utumwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (kutoka Maktaba)
UN Photo/Mark Garten)
Mnyororo wa pingu uliotumika kufungia watumwa ukiwa sehemu ya maonesho kuhusu biashara ya utumwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (kutoka Maktaba)

Lazima kushikamana 

Siku ya Kimataifa ni wakati wa kujifunza na kutafakari juu ya hadithi hizo na kuwaenzi mamilioni ya waafrika ambao walitengwa kutoka kwa nchi na jamii zao, na kusimama kwa mshikamano dhidi ya ubaguzi wa rangi kila mahali." 

Ubaguzi na kutengwa 

Leo, watu wenye asili ya Kiafrika "wanaendelea kukabiliana na ubaguzi wa rangi, kutengwa na kutengwa," alisema. 

Ukosefu wa usawa wa kisiasa, kiuchumi na kimuundo ambao ulijikita katika utawala wa kikoloni, utumwa na unyonyaji, unaendelea leo kukataa usawa wa fursa na haki. 

Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu amewataka watu wote kusimama kidete kupinga ubaguzi wa rangi leo na kila siku. 

Tutokomeze janga hili la kimataifa’ 

Katika ujumbe wake, Rais wa Baraza Kuu Abdulla Shahid amesisitiza haja ya kujadili urithi wa utumwa, hasa katika kutengwa kwa watu wa asili ya Kiafrika, ambao bado wananyimwa haki na usawa. 

"Hebu tusimame kwa mshikamano, tukiungana dhidi ya ukosefu huu wa usawa. Sura hii ya giza haipaswi kupakwa chokaa kamwe". Amesisitiza. 

Natalia Kanem, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na linalojishughulisha na kuendeleza afya ya uzazi na haki za kijinsia pamoja na kukomesha unyanyasaji wa kijinsia, UNFPA, amesema kwamba wakati akiwakumbuka waathiriwa wa utumwa na biashara ya utumwa ya karne nyingi katika bahari ya Atlantiki, "tuungane kutokomeza janga hili la kimataifa la ubaguzi wa rangi”.