Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa laanzishwa mtandaoni kuongeza ufahamu wa uhusiano kati ya tabianchi na afya

WMO na WHO wamezindua jukwaa la ufahamu wa uhusiano kati ya afya na tabianchi.
WHO
WMO na WHO wamezindua jukwaa la ufahamu wa uhusiano kati ya afya na tabianchi.

Jukwaa laanzishwa mtandaoni kuongeza ufahamu wa uhusiano kati ya tabianchi na afya

Afya

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la afya ulimwenguni, WHO na la hali ya hewa, WMO leo yamezindua jukwaa maalum la kuongeza ufahamu juu ya uhusiano kati ya tabianchi na afya, likiwa ni jukwaa la kwanza kabisa la aina yake.

Taarifa ya pamoja iiyotolewa na mashirika hayo jijini Geneva, Uswisi inasema uzinduzi umefanyika kwa kuungwa mkono pia na wakfu wa kampuni ya kutengeneza dawa, WELLCOME na hatua hii inatokana na ongezeko la wito wa kuweko kwa taarifa za kuwezesha watu kuchukua hatua kujilinda dhidi ya athari za kiafya zitokanazo na madhara ya tabianchi na hatari nyingine za kimazingira.

Tabianchi na Afya ni sawa na Ambari na Zinduna

WHO na WMO yanasema tabianchi na afya vina  uhusiano mkubwa au ni saw ana ambari na zinduna. Mabadiliko ya tabianchi, matukio ya hali ya hewa za kupitiliza na uharibifu wa mazingira vina madhara makubwa katika afya ya binadamu na ustawi wake.

Hivi sasa watu wengi zaidi wanakumbwa na madhara ya kiafya yatokanayo na tabianchi, kuanzia maji yasiyo safi na salama, hewa chafu, magonjwa ya kuambukikza na shinikizo kutokana na joto kali.

"Mabadiliko ya tabianchi yanasababisha vifo vya watu wengi hivi sasa,” amesema Diamid Campbell Lendrum, Mratibu wa afya na tabianchi katika WHO, akiongeza “inaathiri mambo muhimu ya msingi tunayohitaji ili tuishi: hewa safi, maji safi, chakula na makazi – na madhara makubwa yanakumba watu walio hatarini zaidi. Kama hakuna hatua za kuchukua kupunguza madhara, basi maendeleo tuliyopata kwenye miongo kadhaa iliyopita yatatoweka. Kupunguza madhara yake kunahitaji sera zenye shuhuda zikiungwa mkono na sayansi na mbinu zilizoko.”

Ametaja mfano wa matumizi ya mifumo ya kutoa onyo mapema kuhusu joto kali, uwezo wa kutabiri mlipuko wa magonjwa.

Jukwaa lina kitu gani?

WMO na WHO wameandaa jukwaa hili la kupata ufahamu na linaweza kutumiwa na wataalamu wa afya, mazingira na tabianchi.

Watumiaji wataweza kuunganishwa na wataalamu mbalimbali duniani wa masuala ya afya, tabianchi na mazingira na wanaweza pia kuona matukio yajayo, taarifa, takwimu, mifano, madhara ya tabianchi kwa afya na kadhalika.

“Mara kwa maraa tunazungumzia wataalamu wa afya ambao wana hoof kuhusu madhara ya mazingira kwenye afya ambayo wao wanashuhudia au wanakutana nayo. Lakini wanakosa mahali pa kupata mafunzo na taarifa za tabianchi mahsusi kwa kile wanachokumbana nacho,” amesema Joy Shumake-Guillemot, anayeongoza ofisi ya pamoja ya WHO na WMO.

“Na kwa upande mwingine tuna wataalamu wa tabianchi ambao wamekalia tafiti na nyaraka muhimu ambazo zinaweza kutumika kufanikisha malengo ya afya lakini hawana fursa ya kufikia watu.”

Jukwaa hili litakuwa linaongezwa taarifa mpya kila wakati pamoja na makala kwenye miezi na miaka ijayo ili kuweza kupanua wigo wa taarifa zinazotakiwa na pia kukidhi mahitaji ya watumiaji.