Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fursa za ajira zazidi kupungua duniani, ILO yatoa mapendekezo

Esther Karisa ni mnufaika wa mradi wa KYEOP unaofadhiliwa na Benki ya Dunia nchini Kenya wenye lengo la kuwasaidia vijana kupata utaalamu na kujitafutia ajira.
Benki ya Dunia
Esther Karisa ni mnufaika wa mradi wa KYEOP unaofadhiliwa na Benki ya Dunia nchini Kenya wenye lengo la kuwasaidia vijana kupata utaalamu na kujitafutia ajira.

Fursa za ajira zazidi kupungua duniani, ILO yatoa mapendekezo

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO limetoa ripoti yake ikisema ukosefu wa ajira na ukosefu wa usawa vyote vitaendelea kuongezeka duniani kutokana na majanga lukuki yanayoingiliana ya kiuchumi na kisiasa na hivyo kutishia kukwamuka kwa soko la ajira duniani.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inaonesha kuwa mwelekeo wa soko la ajira duniani umekuwa mbaya zaidi katika miezi ya karibuni na mwelekeo wa nafasi za ajira utapungua sambamba na kiwango cha ukuaji wa ajira duniani kwenye robo ya mwisho ya mwaka huu wa 2022 iliyoanza mwezi huu wa Oktoba.

Ikipatiwa jina la Ufuatiliaji wa Sekta ya Ajira duniani, ripoti inasema vita ya Ukraine, pamoja na ongezeko la mfumuko wa bei vinasababisha kuporomoka kwa viwango halisia vya ujira kwenye nchi nyingi duniani, na hii inaambatana na kuporomoka kwa ujira kwa kiasi kikubwa wakati wa janga la COVID-19, ambalo limeathiri zaidi makundi ya kipato cha chini.

Ukosefu wa ajira unadhihirika zaidi madhara yake kwenye ongezeko la bei za vyakula na nishati, uchumi unadorora na fursa za maboresho ya kisera zinapungua.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert Houngbo anasema majawabu ya kutatua hali ya sasa ya ajira na kuepusha hali kuwa mbaya zaidi kutahitaji sera za kina na zinazoingiliana na ambazo pia zina mizania kitaifa na kimataifa.

Amesema “tunahitaji utekelezaji wa sera nyingi nap ana ikiwemo será za kuingilia kati kupunguza bei za vyakula, kugawana vema mapato ambayo hayakutarajiwa, kuimarisha hifadhi ya jamii na sera mahsusi za kulenga watu walio hatarini zaidi.