Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirika baina ya UN na Rwanda umekuwa wa changamoto na mafanikio: UN/Rwanda

Maxwell Gomera Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda
UN RWANDA
Maxwell Gomera Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda

Ushirika baina ya UN na Rwanda umekuwa wa changamoto na mafanikio: UN/Rwanda

Wanawake

Serikali ya Rwanda kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa nchini humo wameamua kuitumia siku ya Umoja wa Mataifa kusherekea pia miaka 60 ya Rwanda tangu kujiunga rasmi na Umoja wa Mataifa.  

Flora Nducha wa idhaa ya kiswahili ya Umoja wa Mataifa ameshuhudia maadhimisho hayo yaliyofanyika katika hoteli ya serena mjini Kigali ambako maadhimisho ya 60 ya Rwanda kujiunga na Umoja wa Mataifa yanafanyika.

Flora ameeleza kushuhudia ukumbi ukiwa umesheheni kwa mapambo na watu mbalimbali walioalikwa kuhudhuria maadhimisho haya yaliyoandaliwa kwa pamoja na Umoja wa Mataifa na serikali ya Rwanda yakibeba maudhui “Ushirikiano kwa ajili ya mustakbali bora wa pamoja kwa wote” 

Rwanda inasherekea miaka 60 katika Umoja wa Mataifa
UN RWANDA

Miongoni mwa wageni waalikwa ni wawakilishi wa asasi za kiraia, mawaziri kutoka serikali ya Rwanda, wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa , mabalozi wa nchi mbalimbali walioko Rwanda, waku wa makampuni ya sekta binafsi na wanazuoni. 

Akifungua maadhimisho hayo kwa niaba ya Umoja wa Mataifa kaimu mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini hapa ambaye pia ni mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP Maxwell Gomera amesema  

“Miaka 60 iliyopita serikali ya Rwanda ilikaribishwa kwenye Umoja wa Mataifa moja ya mashirika ya kipekee duniani, likijizatiti kutatua changamoto za pamoja kupitia ushirikiano na hatua za pamoja . Kwa kufanya hivyo serikali ilikuwa inasisitiza lengo lake la kutatua masuala ya ukosefu wa haki , kudumisha amani , usalama na afya ya wananchi miongoni mwa mengine. Miaka 28 iliyopita lengo hilo lilikabiliwa na changamoto kubwa na dunia ilishuhudia muaji mabaya zaidi ya kimbari dhidi ya Watutsi. Hivi karibuni Katibu Mkuu Antonio Guterres alitafakari wakati huo na kushindwa kwetu kama jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kuzuia na kukomesha mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi. Ingawa hatukupitia machungu yenu, ndugu waziri tunatumai mtaturuhusu kufanya kazi nanyi katika safari yenu kuhakikisha asilani hayatatokea tena” 

Vicent Biruta - Waziri wa Mambo ya nje wa Rwanda
UN RWANDA
Vicent Biruta - Waziri wa Mambo ya nje wa Rwanda

Naye Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Rwanda Vincent Biruta akizungumza kwa niaba ya serikali kwenye hafla hii amesema 

“Miaka 60 ya historia ya pamoja imeghubikwa na machungu lakini pia hadithi za mafanikio na mambo ya kujifunza ambayo yanatuhamasisha kuendeleza ushirikiano wetu kwa ajili ya mustakbali bora na wa pamoja kwa wote. Licha ya mazingira magumu tumejifunza kutokana na yaliyopita na tumechagua kuganga yajayo na mazuri tutakayoweza kutimiza kwa kushirikiana kikamilifu kama wanachama wa jumuiya ya kimataifa. Rwanda sasa ni taifa lililoungana na lenye maono mengi asante kwa watu wa Rwanda lakini pia asante kwa ushirikiano na jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa ambao umechukua mtazamo wa maendeleo tangu miaka 28 iliyopita.” 

Sherehe hizi zimeambatana pia na mijadala kuhusu mada mbalimbali ikiwemo masuala ya ulinzi wa amani na mchango wa Rwanda kwenye operesheni za Umoja wa Mataifa, utatuzi wa migogoro na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDG’s. 

Rwanda ilijiunga rasmi kwenye Umoja wa Mataifa tarehe 18 Septemba mwaka 1962 mara tu baada ya kujinyakulia uhuru wake kutoka kwa Wabelgiji. 

Nikiripoti kutoka Serena Hotel mjini Kigali Rwanda mimi ni Flora Nducha wa UN News Kiswahili.