Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN ni tunda la matumaini, turejeshe matumaini hayo, asema Guterres leo siku ya Umoja wa Mataifa

Utiaji saini wa Katiba au Chata ya UN tarehe 26 mwezi Juni mwaka 1945  kwenye jengo la maveterani huko San Fransisco, Marekani.
UN Photo/Yould
Utiaji saini wa Katiba au Chata ya UN tarehe 26 mwezi Juni mwaka 1945 kwenye jengo la maveterani huko San Fransisco, Marekani.

UN ni tunda la matumaini, turejeshe matumaini hayo, asema Guterres leo siku ya Umoja wa Mataifa

Masuala ya UM

Ikiwa leo ni maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni wakati muhimu wa kurejesha tena matumaini na imani katika kile ambacho ubinadamu unaweza kufanikiwa pindi jamii yote ya kimataifa itakapofanya kazi kama kitu kimoja na kwa mshikamano wa kimataifa

Siku ya Umoja wa Mataifa huadhimishwa tarehe 24 ya mwezi Oktoba kila mwaka kukumbuka tarehe kama hiyo mwaka 1945 wakati Chata ya kuanzisha Umoja huo ilipoanza kutumika baada ya kutiwa saini na kuridhiwa na nchi waanzilishi 51 zikiwemo tano zenye ujumbe wa kudumu katika Baraza la Usalama ambazo ni China, Ufaransa, Uingereza, Urusi na Marekani.,

Katibu Mkuu Guterres katika ujumbe wake wa siku hii anasema Umoja wa Mataifa ni tunda la matumaini. Matumaini na azma baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia ya kwamba kusonga kutoka mizozo na kuelekea katika ushirikiano wa kimataifa.

Guterres amesema “leo hii shirika letu linakumbwa na majaribu kuliko wakati wowote ule. Lakini Umoja wa Mataifa uliundwa kwa ajili ya nyakati kama hizi. Sasa kuliko wakati wowote ule tunahitaji kurejesha tena uhai wa misingi ya Chata ya Umoja wa Mataifa katika pembe zote za dunia.”

Walinda amani wa MONUSCO kutoka Tanzania wakiwa na wanawake wenyeji wa DRC.
© MONUSCO
Walinda amani wa MONUSCO kutoka Tanzania wakiwa na wanawake wenyeji wa DRC.

Turejeshee uhai misingi ya Chata ya  UN

Misingi mikuu saba ya Umoja wa Mataifa  ambao sasa una wanachama 193 ni pamoja na kila nchi mwanachama ni sawa na mwingine na migogoro yote inapaswa kutatuliwa kwa njia ya amani.

Katibu Mkuu anasema hilo lifanyike kwa kupatia fursa amani na kwa kumaliza migogoro ambayo inavuruga maisha, mustakabali na maendeleo ya dunia.

Halikadhalika kwa kufanya kazi kutokomeza lindi la  umaskini, kupunguza ukosefu wa usawa na kunusuru malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Ametaja pia kulinda sayari dunia, ikiwemo kuondokana na uraibu wa matumizi ya nishati kisukuku na kuanza kutekeleza mapinduzi ya nishati jadidifu isiyoharibu mazingira.

Hatimaye kuweka mizania ya fursa na uhuru kwa wanawake na wasichana na kuhakiksha haki zao kibinadamu zinazingatiwa.

Malengo ya UN ni manne

Wakati Chata ya Umoja wa Mataifa ina misingi saba, kwa upande wa malengo  yake ni manne ambayo ni kulinda amani na Usalama duniani, kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina ya nchi, kufanikisha ushirikiano wa kimataifa katika kutatua matatizo ya kiuchumi, kijamii, kitamaduni au kiutu na kuwa kitovu cha kuweka utangamano wa vitendo vya nchi katika kufanikisha malengo hayo.