Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malkia Máxima atembelea Tanzania kujionea maendeleo ya huduma za kifedha za kidijitali

Mchechemuzi Maalum wa Katibu wa UN kuhusu ujumuishi wa kifedha kwa maendeleo, Malkia Maxima wa Uholanzi akisalimiana na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es salaam.
UN Tanzania
Mchechemuzi Maalum wa Katibu wa UN kuhusu ujumuishi wa kifedha kwa maendeleo, Malkia Maxima wa Uholanzi akisalimiana na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es salaam.

Malkia Máxima atembelea Tanzania kujionea maendeleo ya huduma za kifedha za kidijitali

Ukuaji wa Kiuchumi

Mchechemuzi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya ujumuishi wa kifedha kwa ajili ya Maendeleo UNSGSA Malkia Máxima Zorreguieta wa Uholanzi amefanya ziara ya siku tatu nchini Tanzania kuanzia tarehe 17 mwezi huu wa Oktoba kujionea maendeleo ya nchi hiyo katika huduma za fedha kidijitali. 

Takwimu za Kundi la Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa asilimia 52 ya watu wazima nchini Tanzania sasa wana akaunti ya benki.  Ilikinganishwa miaka ya 2011 na 2021, taasisi ya Takwimu ya Global Findex  inaonesha kuna tofauti ya asilimia 17 tu.

Idadi ya wanawake wenye akaunti ya kidijitali ni ndogo

Ongezeko hilo kwa kiasi fulani linaelezewa kutokana na sababu ya watu wengi kuwa na akaunti ya kidijitali.  Takwimu hizo pia zinaonesha uwepo wa pengo kati ya wanaume na wanawake wenye akaunti ambayo ni asilimia 13, hali inayoleta madhara kwa wanawake.

Wakati wa ziara yake, Malkia Máxima alizungumza na wawakilishi wa serikali, mashirika ya maendeleo ya kimataifa, taasisi za fedha, mashirika ya teknolojia ya kifedha ama fintech na mashirika yasiyo ya kibiashara ambapo alizungumza na wahusika wakuu kuhusu kile kinachohitajika ili kuunganisha watu wasiojiweza zaidi na huduma za kifedha na kuwawezesha kushiriki katika uchumi jumuishi wa kidijitali.

“Tunajua kupitia ziara yangu hii tutawaleta pamoja zaidi sekta binafsi na ya umma pamoja na serikali ili kuhakikisha wananchi wanatumia huduma za kifedha asilimia 100 na watu wengi wanaweza kuzifikia huduma hizo na kuwahakikishia kipato, mnepo na kuweka bima na akiba ili hata pale kunapotokea na msukosuko wa kiuchumi waweze kujikimu na kujiongezea fursa.” Alisema Malkia Maxima

Ziara mkoani Kilimanjaro

Katika ziara yake nchini Tanzania, Malkia Maxima alitembelea kijiji cha Uduru makoa kilichopo Wilaya ya Siha, mkoa wa Kilimanjaro ambapo alikutana na wakulima wanaonufaika na mradi wa acre fund unaowapa bima ya kilimo na ufugaji.

Wakulima waliojiunga na mradi huo walimfahamisha Malkia kwamba waliweza kunufaika na fedha za kijikimu, kulipa ada za watoto na kupata fedha za kununua mbegu za msimu uliofuatia wa kilimo pamoja na kunufaika na matumizi ya mbegu bora zinazozalisha zaidi.

Bima kwa wakulima

Mwakilishi huyo Maalum wa Katibu Mkuu, alizungumza na waanzilishi pamoja na wakulima wa ndani kuhusu bidhaa za bima za ACRE Afrika. Shirika hili hutumia taarifa na takwimu za hali ya hewa kutoka kwenye satelaiti na vituo vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe kukadiria hali ya shamba na uharibifu unaowezekana kwa mavuno.

Wakulima, hao wanaomiliki mashamba yao binafsi, hupewa kadi maalum za kukwangua ambazo hujazwa kiwango cha kuweka bima ya mazao yao dhidi ya ukame au mafuriko  kulingana na bajeti na mahitaji yao. Baadae wao hupata malipo ya bima bila hata kudai.