Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na wadau wazindua ombi la dola milioni 145.6 kuipiga jeki Haiti

Mwanamke anayeugua kipindupindu akipatiwa matibabu kwenye hospitali moja katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince
© UNICEF/Odelyn Joseph
Mwanamke anayeugua kipindupindu akipatiwa matibabu kwenye hospitali moja katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince

UN na wadau wazindua ombi la dola milioni 145.6 kuipiga jeki Haiti

Afya

Serikali ya Haiti imeungana na Umoja wa Mataifa na washirika wa masuala ya kibinadamu kuzindua ombi la dola milioni 145.6 kusaidia kukabiliana na dharura ya ugonjwa wa kipindupindu nchini humo na kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa watu milioni 1.4 wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi. 

Baada ya zaidi ya miaka mitatu bila kisa cha kipindupindu kilichoripotiwa nchini Haiti, mamlaka ya kitaifa tarehe 2 Oktoba iliripoti visa viwili vipya vilivyothibitishwa vya kipindupindu katika mji mkuu wa Port-au-Prince. 

Kufikia Jumatatu wiki hii, wizara ya afya ya umma na idadi ya watu imeripoti kesi 8,708 zinazoshukiwa, na wagonjwa 802 waliothibitishwa, huku kukiwa na vifo 161 kote nchini. 

Mtoto akitembea kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince
UNDP Haiti/Borja Lopetegui Gonzalez
Mtoto akitembea kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince

Kipindupindu kinaweza kuzuilika na kutibiwa 

"Kipindupindu ni ugonjwa unaoweza kuzuilika na unaoweza kutibika, na kwa kuzingatia uzoefu na utaalamu wao, taasisi za kitaifa ziliweka pamoja mkakati wa kukabiliana na hali hiyo kwa kuungwa mkono na jumuiya nzima ya kibinadamu ya ndani ya nchi na ya kimataifa," amesema mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa na misaada ya kibinadamu, Ulrika Richardson. 

Ameongeza kuwa "Hata hivyo kuongezeka kwa wagonjwa katika wiki za hivi karibuni na kuenea kwa kasi kwa kipindupindu nchini kunatia wasiwasi." 

Watu 500,000 wako hatarini 

Kulingana na shirika la afya la nchi za Amerika PAHO na WHO, watu 500,000 wako katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo. 

Wagonjwa wa kipindupindu wakipata huduma kwenye kituo kimoja cha afya kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince
© UNICEF/Odelyn Joseph
Wagonjwa wa kipindupindu wakipata huduma kwenye kituo kimoja cha afya kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince

Mgogoro wa kipindupindu umeathiri zaidi idadi ya watu ambao tayari wako hatarini.  Na mashirika hayo yamesema uchambuzi wa hivi karibuni wa uhakika wa chakula nchini Haiti unaonyesha kuwa watu milioni 4.7, karibu nusu ya idadi ya watu wote nchini humo, wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula, huku watu 19,200 wakiishi katika hali rasmi ya njaa, ikiwa ni mara ya kwanza hii kutokea katika historia ya hivi karibuni. 

Raia wa Haiti pia wanakabiliwa na kuongezeka kwa ghasia kutokana na shughuli uhalifu za magenge yenye silaha.  

Magenge haya hutumia unyanyasaji wa kijinsia kama silaha ya kutisha watu na kupata udhibiti wa maeneo. 

Takriban watu 100,000 wamekimbia makazi yao tangu Juni 2021 baada ya kukimbia ghasia. 

Utawala wa magenge 

Barabara kuu zinazounganisha mji mkuu na maeneo mengine ya nchi ziko chini ya udhibiti au ushawishi wa magenge, ambayo yamepunguza au hata kuwanyima raia kupata huduma za msingi kwa miezi mingi. 

Katika muktadha huu, wasaidizi wa masuala ya kibinadamu wanategemea usafiri mbadala wa gharama nafuu ili kuendelea kutoa msaada kote nchini, ambao ni pamoja na vita dhidi ya kudhibiti kipindupindu. 

Umoja wa Mataifa na washirika wanatoa wito wa ufadhili kusaidia juhudi zinazoongozwa na serikali za kutoa maji safi, huduma za kujisafi na usafi wa mazingira, na shughuli za afya, huku wakishughulikia mahitaji ya dharura ya chakula, lishe na ulinzi.