Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa kusoma na kuhesabu waleta manufaa kwa wanafunzi nchini Zambia

Vifaa vya kuchezea na kujifunzia watoto vilivyotengenezwa na watumishi wa kujitolea nchini Zambia kwa ajili ya kutumiwa na watoto kwenye vituo vya maendeleo ya mapema ya mtoto, ECD vinavyoendeshwa na UNICEF Zambia.
© UNICEF/Kinny Siakachoma
Vifaa vya kuchezea na kujifunzia watoto vilivyotengenezwa na watumishi wa kujitolea nchini Zambia kwa ajili ya kutumiwa na watoto kwenye vituo vya maendeleo ya mapema ya mtoto, ECD vinavyoendeshwa na UNICEF Zambia.

Mradi wa kusoma na kuhesabu waleta manufaa kwa wanafunzi nchini Zambia

Utamaduni na Elimu

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya watoto UNICEF nchini Zambia kwa kushirikiana na serikali ya Zambia na Taasisi ya Hampel wanaendesha programu iitwayo Catch Up yenye lengo la kuwasaidia wanafunzi wa shule za msingi nchini humo kupata matokeo bora ya masomo ya hisabati na kusoma hususan wale waliokuwa na ufaulu mdogo wa masomo hayo na sasa matokeo chanja yameanza kuonekana.

Katika jimbo la Luapula nchini Zambia, video ya UNICEF inamuonesha mwalimu akitumia mbinu mbali mbali ikiwemo kutumia ubao , kuchora kwenye sakafu na chaki na hata kurusha mawe ili kuwaelimisha wanafunzi somo la hisabati.

Wanafunzi hawa ni miongoni mwa zaidi ya wanafunzi 80,000 wanaopata masomo ya ziada ya somo hili la hisabati lakini likiwa na mbinu pia za kuwafanya wajue kusoma kupitia programu ya Catch up. Judith Chama ni mwalimu wa programu hiyo katika shule ya msingi Chiseta anasema hapo awali hali ilikuwa si nzuri

“Kabla ya kuja kwa program ya Catch up, wanafunzi wetu walikuwa hawawezi kusoma nambari kama elf umoja na mbili, lakini baada ya kuanza kwa masomo mpaka sasa, wanafunzi ambao nipo nao darasani kwangu wanaweza kusoma 5366.”

Katika shule nyingine ya msingi ya Pembeshi mwalimu Caroline Nsemiwe anasema mzazi wa mtoto mmoja alimpa ushuhuda kuwa mwanae ameimarika sana kwenye kusoma, hapo awali alikuwa anasoma herufi moja moja lakini sasa anaweza kusoma neno kamili.
Kauli yake hii inaungwa mkono na wazazi Esther Bwalya “Nikiangalia mtoto wangu alipokuwa awali na alipo sasa napata furaha sana, kuna utofauti mkubwa.

Na mzazi mwingine ni  Akim Mulenge “Watoto wetu wangekuwa nyuma sana kama wasingefikiwa na program hii mapema kwasababu Watoto walio darasa la 3,4 na la 5 wanafanya vizuri zaidi kuliko wale walio darasa la 6 na 7”.

Habari hizi njema pia zinawapa furaha wafadhili wa mradi huo na kupongeza ushirikiano wanaopata kutoka kwenye uongozi wa jimbo la Luapula na wanaaamini matokeo hayo yatakuwa na manufaa bora zaidi kadri siku zinavyozidi kwenda.

Kwa sasa programu hii inatekelezwa katika wilaya nne za jimbo la Luapula, na mwaka 2023 inategemewa kuanza kutekelezwa katika wilaya zote za jimbo hilo.