Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Mabenchi ya Urafiki' yatakayotumika wakati wa Kombe la Dunia la FIFA Qatar 2022, yazinduliwa

Sheikha Hind na Sir Mo Farah wakizindua benchi la Uingereza (moja ya mabenchi ya Urafiki) wakati wa Mkutano wa Dunia wa Ubunifu wa Afya.
WHO
Sheikha Hind na Sir Mo Farah wakizindua benchi la Uingereza (moja ya mabenchi ya Urafiki) wakati wa Mkutano wa Dunia wa Ubunifu wa Afya.

'Mabenchi ya Urafiki' yatakayotumika wakati wa Kombe la Dunia la FIFA Qatar 2022, yazinduliwa

Afya

Mradi wa kipekee unaohusisha mabenchi ya umma yaliyotengenezwa maalum ili kuhamasisha umuhimu mkubwa wa afya ya akili, na jukumu ambalo kandanda na michezo inaweza kutekeleza kwa upana zaidi ili kukuza afya ya akili, umetangazwa leo. 

"Mabenchi 32 ya Urafiki" - moja kwa kila taifa linaloshiriki Kombe la Dunia la FIFA Qatar 2022  yamejengwa kwa ajili ya kuwekwa katika maeneo maarufu ya mji wa Doha nchini Qatar, ikiwa ni pamoja na maeneo ya viwanja vya mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Jumapili, Novemba 20, 2022  hadi Jumapili Desemba 18, 2022. 

Mradi huo ni sehemu ya ushirikiano wa ‘Michezo kwa Afya’, unaoongozwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani na Wizara ya Afya ya Umma ya Qatar (MoPH). Lengo lake ni kuonesha umuhimu wa afya ya akili na kutoa ushauri kuhusu njia za kukuza ustawi wa akili, ikiwa ni pamoja na kupitia umuhimu wa shughuli za kimwili na michezo. Mpango huo unaungwa mkono na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani, FIFA, Kamati Kuu ya Uwasilishaji na Urithi, WISH, Shirika lisilo la kiserikali la [Friendship%20Benches]Benchi za Urafiki na Ushirikiano wa Afya kwa Wote wa WHO

Sanjari na Siku ya Afya ya Akili Duniani, baadhi ya mabenchi ya kwanza yamewasilishwa leo katika Uwanja wa 974 (974 Stadium), mjini Doha, mojawapo ya viwanja vya Kombe la Dunia la FIFA la mwaka huu. Mpango wa benchi umezinduliwa kwa njia ya mfano kwa benchi ya Uingereza katika hafla ya afya ya kimataifa ya Wakfu wa Qatar, Mkutano wa Dunia wa Ubunifu wa Afya (WISH) katika utangulizi wa uoneshaji mkubwa wa mabenchi kwenye Siku ya Afya ya Akili Duniani. 

Mwanariadha Mwingereza Sir Mo Farah, ambaye medali zake 10 za dhahabu za Olimpiki na Ubingwa wa Dunia zimemfanya kuwa mwanariadha mwenye mafanikio zaidi katika mbio za wanaume kuwahi kutokea, ameshiriki kuzindua benchi la Uingereza mjini Doha, ambapo ameungana na Sheikha Hind bint Hamad Al Thani, Makamu Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Qatar kwa ajili ya michezo na afya ya akili. 

"Kukutana na Sir Mo na kusikia hadithi ya kuvutia ya jinsi alivyoondoka Mogadishu kwenda London akiwa mvulana mdogo na changamoto za afya ya akili alizokabiliana nazo zilionesha umuhimu wa kukaa chini na kuzungumza kuhusu afya yetu ya akili," anasema Sheikha Hind na kuongeza akisema, "Ninajivunia kwamba mpango wa afya wa kimataifa wa Wakfu wa Qatar (Qatar Foundation) ni kati ya wale wanaosaidia kuangazia afya ya akili kwa njia ya ubunifu na ya vitendo." 

Mradi wa mabenchi unaendana na malengo na kampeni za kawaida za kila shirika mdau, ikijumuisha kampeni ya FIFA-WHO ya #REACHOUT, Mradi wa "Je, Uko sawa?" na mradi wa kwanza wa Mabenchi ya Urafiki wenyewe, ambao awali ulianzia nchini Zimbabwe na kuungwa mkono na WHO. Tukio la WISH hapo awali pia lilitumika kama jukwaa la kukuza dhana ya Mabenchi ya Urafiki. Mpango huu pia unalenga kukuza shughuli za kimwili kama mojawapo ya matokeo muhimu ya mradi wa Michezo na Afya. Kwa hili kipengele maalum kinachoonekana kwenye kila benchi ni vielelezo vyenye ushauri unaoelezea mazoezi rahisi na yenye ufanisi ambayo wageni wanaweza kufanya kwa ajili ya afya zao za kimwili. 

"Benchi ni chombo rahisi lakini chenye nguvu kwa ajili ya kukuza afya ya akili, kutoka kwenye viti vya bustani za kupumzika ambapo watu hukusanyika hadi kwenye viwanja vya mpira ambapo wachezaji na wafanyakazi hutazama timu zao zikicheza kwa furaha na ahadi ya michezo na mafanikio," amesema Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi wa WHO.  

Ghebreyesus ameongeza kusema, “mradi wa Mabenchi ya Urafiki ni ukumbusho wenye nguvu wa jinsi afya, kuanzia kiakili hadi afya ya kimwili, ni ya thamani na ya kawaida kwa watu na mataifa yote, na jinsi, kupitia michezo, watu wanaweza kufikia wengine, kama wanadamu wenzao, katika hali ya mshikamano na msaada.” 

Maeneo ambako kila benchi kati ya hayo 32 yatawekwa, yatatangazwa hivi karibuni. Wageni wataweza kutembelea mabenchi ya mataifa yao na mengine katika kuonesha kunga mkono uhamasishaji wa afya ya akili.