Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa ILO waleta matumaini kwa watamil nchini Sri Lanka

Bi. Krishnakumar Jeyaranjini, mnufaika wa mradi wa ILO wa kujengea uwezo wa kiuchumi kaya zinazoongozwa na wanawake nchini Sri Lanka hasa maeneo yaliyokuwa yameathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
ILO
Bi. Krishnakumar Jeyaranjini, mnufaika wa mradi wa ILO wa kujengea uwezo wa kiuchumi kaya zinazoongozwa na wanawake nchini Sri Lanka hasa maeneo yaliyokuwa yameathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mradi wa ILO waleta matumaini kwa watamil nchini Sri Lanka

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Sri Lanka, serikali na mradi wa pamoja wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya amani kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO, wanatekeleza mradi wa kuinua jamii za watamil ambazo zimerejea kwenye makazi yao baada ya mzozo wa muda mrefu kaskazini mwa nchi hiyo, mradi ambao unawezesha jamii kujumuika tena na kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi na kuinua kipato chao baada ya mzozo uliodumu kwa takribani miaka 25.

Wanufaika wa mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Marekani ni kaya zinazoongozwa na wanawake, vijana walioathiriwa na mzozo pamoja na watu wenye ulemavu.

Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO mnufaika mmoja wa mradi huo ni Udayakumar Utharshin ,mwanamke mwenye umri wa miaka 28 ambaye vita vilisababisha akimbie makazi yake, lakini sasa amerejea na walipatiwa mafunzo ya jinsi ya kuchakata makumbi ya nazi kuwa nyuzi nyuzi za kujaza kwenye samani na magodoro ya vitanda.

Sasa anamiliki kiwanda na anasema, katika kiwanda hiki tumeajiri watu 45. Kati yao hao wanawake ni 43 na wanaume ni wawili tu. Tumeajiri zaidi watu wenye ulemavu, wanawake wanaoongoza kaya zao na watu maskini, kwa sababu jamii nyingi hapa ni maskini. 

Bi. Utharshin ambaye alijeruhiwa wakati wa mzozo wa Tamil anasema awali ilikuwa ni vigumu kwa watamil kupata ajira lakini sasa kupitia mradi huu jamii hizi zinapata ajira tena zenye staha.

Mnufaika mwingine ni mkulima wa karanga, Issakimuthu Selvakumar mwenye umri wa miaka 56 ambaye anatumia mguu mmoja wa bandia kwa kuwa wakati wa vita alipigwa na kombora na kupoteza mguu wake.

Bwana Selvakumar anasema ILO ilitukusanya na kutupatia kilo 20 za karanga kwa ajili ya kupanda. Tulivuna mara nane zaidi ya kiwango hicho. Kisha wakatugejengea kisima cha maji. Sasa tunalima mwaka mzima badala ya zamani ambapo tulilima msimu wa mvua pekee mwezi Machi. Na sasa watajenga kiwanda cha kuchakata karanga kwa hiyo tutauza mavuno yote. Hii itakuwa na faida kwetu.”