Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sri Lanka: Kipindi cha mpito kiwe cha amani na mchakato uwe jumuishi- UN

Sri Lanka inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta wakati huu ambapo taifa hilo limegubikwa na janga la kiuchumi
WFP
Sri Lanka inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta wakati huu ambapo taifa hilo limegubikwa na janga la kiuchumi

Sri Lanka: Kipindi cha mpito kiwe cha amani na mchakato uwe jumuishi- UN

Amani na Usalama

Kufuatia kujiuzulu kwa Rais wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo Hanaa Singer-Hamdy, amesihi wadau wote wahakikishe kuwa kuna kipindi cha mpito kuelekea serikali kamili na kiwe cha amani na kiheshimu Katiba ya Sri Lanka.
 

Bwana Rajapaksa alijiuzulu jana Alhamisi akiwa Singapore uhamishoni ambako alikimbilia siku ya Jumatano kufuatia miezi kadhaa ya maandamano nchini humo kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani amenukuu taarifa ya Mratibu Mkazi huyo ikisema kuwa ni muhimu kipindi cha mpito wa madaraka kikaambatana na mashauriano mapana na jumuishi ndani nan je ya Bunge.

Amerejelea wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia chanzo au mzizi wa ukosefu wa utulivu nchini Sri Lanka sambamba na machungu yaliyogubika wananchi.

“Mazungumzo na wadau wote ni njie bora zaidi ya kushughulikia shaka na shuku za wananchi na wakati huo huo kukidhi matamanio ya wananchi wote wa Sri Lanka,” amenukuliwa Bi. Singer-Hamdy.

Amesisitiza kuwa mamlaka lazima zihakikishe kuwa katika kusongesha utawala wa sheria na utulivu, vikosi vya usalama ni lazima vijizuie kutumia nguvu na vitekeleze wajibu wao kwa mujibu wa misingi ya haki za binadamu.

Umoja wa Mataifa kwa upande wake uko tayari kusaidia serikali na wananchi wa Sri Lanka katika kushughulikia changamoto za sasa na za muda mrefu.