Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali baini wavumbuzi wa ndani, WIPO iweze kuwatambua

Ombeni Sanga, mvumbuzi kijana mtanzania ambaye ametengeneza kifaa chenye uwezo wa kusambaza elimu katika mazingira ambayo hakuna mwalimu.
UN Tanzania
Ombeni Sanga, mvumbuzi kijana mtanzania ambaye ametengeneza kifaa chenye uwezo wa kusambaza elimu katika mazingira ambayo hakuna mwalimu.

Serikali baini wavumbuzi wa ndani, WIPO iweze kuwatambua

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Eneo la Asia Mashariki limeendelea kutawala katika fani ya uvumbuzi kwenye tasnia ya Sayansi na Teknolojia duniani, limesema hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la haki miliki, WIPO.

Taarifa ya WIPO iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inataja eneo hilo la Asia Mashariki kushika nafasi ya kwanza kati ya nafasi tano za maeneo yanayoongoza duniani kwa uvumbuzi kwenye Sayansi na Teknolojia, WIPO ikisema kichocheo ni nchi kupatia wavumbuzi wake wa ndani fursa ya kuchanua.

Wavumbuzi wa ndani ni kichocheo cha ajira na ukuaji

WIPO imetoa hii leo taarifa tangulizi ya kipimo cha kila mwaka duniani cha uvumbuzi au GII ambapo katika Asia Mashariki, kundi moja la uvumbuzi liko Japan, mawili China, na moja Korea Kusini. Nafasi ya tano imechukuliwa na Marekani.

Ripoti kamili itazinduliwa tarehe 29 mwezi huu wa Septemba na lengo ni kubaini ni eneo gani katika nchi kuna makundi mengi zaidi ya uvumbuzi.

Mathalani kwa taarifa hii ya leo, wavumbuzi wengi wako miji ya Tokyo na Yokohama nchini Japan, ikifuatiwa na Shenzhen, Hong Kong, Guangzhou huko China na Hong Kong, na kisha San Jose, San Francisco nchini Marekani.

Serikali baini wavumbuzi wa ndani ili WIPO iweze kuwatambua

Akinukuliwa kwenye taarifa hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WIPO, Daren Tang amesema, “makundi ya uvumbuzi ndani ya nchi ni muhimu sana katika kuchochea mifumo ya uvumbuzi ya kitaifa.”

Bwana Tang amesema kwa kuwabaini na kuwatambua, itasaidia WIPO kufahamu ni wapi na ni uvumbuzi gani unafanyika na hivyo kusongesha harakati za uvumbuzi kama njia thabiti ya kuchochea fursa za ajira, uwekezaji na ukuaji.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WIPO amesema kando ya kubaini maeneo ya ndani ya uvumbuzi huko Asia, Marekani na Ulaya, wamegundua pia maeneo mapya yanayoinukia ya  uvumbuzi huko Brazil, India, Iran, Uturuki na kwingineko.