Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mawaziri wa Elimu wakutana kujadili faida na changamoto za AI kwenye elimu

Shule kote ulimwenguni zinahimizwa kubuni sera kuhusu matumizi ya programu za AI au akili bandia katika elimu.
© Unsplash/Hitesh Choudhary
Shule kote ulimwenguni zinahimizwa kubuni sera kuhusu matumizi ya programu za AI au akili bandia katika elimu.

Mawaziri wa Elimu wakutana kujadili faida na changamoto za AI kwenye elimu

Utamaduni na Elimu

Ili kukabiliana na uibukaji wa kasi na mpya wenye nguvu wa akili bandia (AI) shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO limefanya mkutano wa kwanza wa kimataifa wa Mawaziri wa Elimu ili kuchunguza fursa za sasa na zijazo, changamoto na hatari ambazo AI inaweza kuleta kwenye mifumo ya elimu.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na UNESCO kutoka Paris Ufaransa imeeleza zaidi ya Mawaziri 40 walishiriki katika mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao na wameeleza mbinu wanazotumia katika sera na mipango yao inayojikita kuangalia namna bora ya kuunganisha AI katika elimu.

Katika mkutano huo uliofanyika tarehe 25 Mei 2023, UNESCO iliwasilisha muongozo wake AI na elimu   ikijumuisha mazungumzo ya wazi yalitotolewa na wadau wengi.

Hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa

Utafiti mpya wa kimataifa uliofanywa na UNESCO kwa zaidi ya shule na vyuo vikuu 450 uligundua kuwa chini ya asilimia 10 ndio wametunga sera za kitaasisi na/au mwongozo rasmi kuhusu matumizi ya AI.

Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kunahitajika kutolewa kwa majibu ya haraka kwa uibukaji wa Akili Bandia kwa kasi kwani program za AI sasa zinaweza kuzalisha au kutoa ubunifu wa maandishi na wa kuona ni hii inaweza kuwa changamoto kwa taasisi.

Pamoja na jukumu muhimu la walimu katika enzi hii mpya kama wawezeshaji wa kujifunza, lakini walimu wanahitaji mwongozo na mafunzo ili kukabiliana na changamoto hizi.

Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Elimu wa UNESCO Stefania Giannini amenukuliwa katika mkutano huo akileza kwamba “kuendelea kutengenezwa kwa aina mbalimbali kwa Akili Bandia (AI) kunafungua upeo mpya na changamoto kwa elimu lakini tunahitaji kuchukua hatua haraka ili kuhakikisha kuwa teknolojia mpya za AI zinaunganishwa katika elimu kwa masharti yetu.

Giannnini ameeleza pia wajibu wa kila wizara ya elimu kuweka kipaumbele kwa usalama, ushirikishwaji, utofauti, uwazi na ubora kama ilivyoelezwa katika Pendekezo lililo tolewa na UNESCO kuhusu Maadili ya Akili Bandia lililopitishwa kwa kauli moja na Nchi Wanachama wetu.

Yaliyoelezwa na mawaziri

Katika majadiliana yao mawaziri walieleza baadhi ya masuala mtambuka ikiwa ni pamoja na jinsi ya kurekebisha mifumo ya elimu kuendana na ukuaji wa haraka wa AI, jinsi ya kuunganisha AI katika mitaala, mbinu za kufundishia na mitihani, na jinsi ya kupunguza dosari asili za teknolojia hizo ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa kufanya makosa ya wazi na kutoa taarifa zenye upendeleo.

Mjadala huo wa mawaziri ulifichua kwamba serikali duniani kote ziko katika mchakato wa kutunga sera zinazofaa kujibu changamoto za AI katika mazingira haya yanayoendelea kukuwa kwa kasi, kuboresha zaidi mikakati ya kitaifa kuhusu AI, kuhusu ulinzi wa taarifa, na mifumo mingine ya udhibiti.

UNESCO kuzindua miongozo ya AI kwenye elimu

UNESCO imeahidi kuendelea kuongoza mazungumzo ya kimataifa na watunga sera, washirika wa Elimu na Teknolojia EdTech, wasomi na mashirika ya kiraia.

Pia wanatengeneza miongozo ya sera kuhusu matumizi ya AI katika elimu na utafiti, pamoja na mifumo ya ujuzi wa AI kwa wanafunzi na walimu kwa elimu ya shule.

Haya yote yanatarajiwa kuzinduliwa wakati wa Wiki ya Kujifunza kwa Kidijitali, ambayo itafanyika katika Makao Makuu ya UNESCO huko Paris mnamo 4-7 Septemba 2023.