Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wenye asili ya Afrika bado wanakabiliwa na ubaguzi wa rangi: Guterres

Siku ya Kimataifa ya watu wenye asili ya Kiafrika yaadhimishwa kwa mara ya kwanza 31 Agosti 2021
PAHO
Siku ya Kimataifa ya watu wenye asili ya Kiafrika yaadhimishwa kwa mara ya kwanza 31 Agosti 2021

Watu wenye asili ya Afrika bado wanakabiliwa na ubaguzi wa rangi: Guterres

Haki za binadamu

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya watu wenye asili ya Afrika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema pamoja na utajiri wa urithi wa utamanduni na mchango mkubwa unaotolewa na watu wenye asili ya Afrika katika jamii lakini bado wanakabiliwa na ubaguzi ulio ota mizizi. 

Huu ni mwaka wa pili tangu kuanza kwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya watu wenye asili ya Afrika ambapo katibu Mkuu Guterres amesema mwezi Desemba mwaka huu kutafanyika kikao cha kwanza cha Jukwaa la Kudumu la Watu Wenye Asili ya Kiafrika na kuhimiza watu wote kujiandaa kushiriki na kusukuma mbele kazi ya Jukwaa.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa “ Duniani kote, mamilioni ya watu wenye asili ya Kiafrika bado wanashuhudia ubaguzi wa rangi uliokita mizizi na wa kimfumo. Ndiyo maana Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa wito wa kuheshimiwa kikamilifu kwa haki zao za kibinadamu na uhuru wao wa kimsingi, kwa ajili ya kurekebisha mambo hayo yanapokiukwa, na kuomba msamaha rasmi na kulipwa kwa makosa makubwa ya utumwa na ukoloni.”

Ameeleza pia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeomba kuwepo na kikosi kazi kitakacho simamia utekelezwaji kwa Ufanisi wa Azimio la Durban na Mpango wa Utekelezaji, kikosi kazi hicho kitaandaa rasimu ya tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu kukuza na kuheshimu kikamilifu haki za binadamu za watu wenye asili ya Afrika.

Amesisitiza kuwa jukwaa litachangia kazi hii muhimu sana na kwamba “ni muhimu kwa pamoja tuendelee kuongea  kwa sauti kubwa na bila kukosa dhidi ya dhana yoyote ya ubaguzi wa rangi na kwamba tufanye kazi bila kuchoka ili kukomboa jamii zote kutoka kwa balaa ya ubaguzi wa rangi.”