Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya kijamii inastahili pia katika uchumi wa kidijitali:UN 

Maendeleo ya teknolojia yamesaidia kituo cha ajira cha Nouakchott, Mauritania kufikiwa watu wengi zaidi wanaosaka ajira
© UNDP Mauritania/Freya Morales
Maendeleo ya teknolojia yamesaidia kituo cha ajira cha Nouakchott, Mauritania kufikiwa watu wengi zaidi wanaosaka ajira

Haki ya kijamii inastahili pia katika uchumi wa kidijitali:UN 

Haki za binadamu

Katika kuadhimisha siku ya haki ya kijamii duniani leo Februari 20, Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa kuziba pengo la kidijitali lililozidishwa na janga la corona au COVID-19 na kuratibu kanuni za kazi katika majukwaa ya kidijitali. 

Uchumi wa kidijitali unabadili ulimwengu wa kazi , na Umoja huo unasema katika muongo mmoja uliopita kupanuka kwa wigo wa watu kuunganishwa na mtandao, matumizi ya kompyuta na data vimesababisha kuzalishwa kwa majukwaa ya kidijitali ambayo yameingia katika sekta nyingi za kiuchumi na katika jamii. 

Tangu kuanza kwa mwaka 2020, athari za COVID-19 zimepelekea kuanzishwa kwa vifaa vya kufanyia kazi nyumbani ambavyo vimeruhusu kuendelea kwa shughuli mbalimbali za kibiashara, na kuimarisha zaidi ukuaji na athari chanya za uchumi wa kidijitali. 

Janga hilo pia “limeanika wazi ongezeko la kupanuka kwa pengo la kidijitali ndani ya nchi zelizoendelea na zinazoendelea, hususan katika upande wa upatikanaji , uwezo wa kumudu na matumizi ya teknolojia za taarifa na mawasiliano (ICTs) na fursa ya kuwa na mtandao wa intaneti pengo ambalo limeongeze kutokuwepo kwa usawa duniani.” 

Umoja wa Mataifa unasema wakati mitandao ya kidijitali inatoa fursa kwa wafanyakazi kujipatia kipato na faida za muondo tofauti wa ufanyajikazi, hususan kwa wanawake , watu wenye ulemavu, vijana na wafanyakazi wahamiaji, pia inaleta changamoto. 

“Kwa upande wa wafanyakazi changamoto hizo zinahusiana na kanuni za kazi na kipato, haki zao za mazingira bora ya kazi, ulinzi wa hifadhi ya jamii na viwango bora vya maisha, matumizi ya ujuzi na haki ya kuanzisha amba kujiunga na vyama vya wafanyakazi.” 

Kanuni za kazi mtandaaoni ziratibiwe 

Athari za janga la za COVID-19 zimeweka bayana hatari na pengo la ushiriki wa wafanyakazi katika majukwaa ya kitijitali . 

Kwa biashara za kiasili changamoto ni pamoja na kutokuwepo usawa katika majukwaa ya ushindani, ambapo baadhi yao hayatozi kodi na mjukumu mengine kutokana na kwamba ni mapya hasa kwa kuzingatia sula la wafanyakazi wake. 

Changamoto nyingine kwa biashara za asili ni fedha zinazohitajika kuweza kuendelea kujikita katika mitandao ya kidijitali hususan kwa wafanyabiashara wadogo na wa wastan na kutokuwa na uhakika wa upatikanaji wa miundombinu ya kidijirtali inayoaminika katika maeneo ya Kusini mwa dunia. 

Maadhimisho ya siku ya haki za kijamii duniani mwaka huu yanaunga mkono juhudi za jumuiya ya kimataifa katika kusaka suluhu za kufikia malengo ya maendeleo endelevu , kutokomeza umasikini, kuchagiza ajira zenye hadhi, ulinzi wa kimataifa wa hifadhi ya jamii, usawa wa kijinsia na fursa ya ustawi wa kijamii na haki kwa wote. 

Hivyo inawachagiza wadau wote kuanzia nchi wanacha, taasisi husika za Umoja wa Mataifa na wadau wengine kuchukua hatua zinazohitajika kukabiliana na pengo la kidijitali , kutoa fursa za ajira zenye hadhi, kulinda haki za kazi na za binadamu katika nyakati hizi za utandawazi wa kidijitali.