Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF imetuepusha na maji yenye wadudu- Wakazi wa Cibitoke

Mtoto akiwa amesimama karibu na pampu ya maji iliyozingirwa na maji ya mafuriko huko Gatumba nchini Burundi.
© UNICEF/Karel Prinsloo
Mtoto akiwa amesimama karibu na pampu ya maji iliyozingirwa na maji ya mafuriko huko Gatumba nchini Burundi.

UNICEF imetuepusha na maji yenye wadudu- Wakazi wa Cibitoke

Msaada wa Kibinadamu

Tukiwa tunaelekea ukingoni mwa wiki ya maji duniani , nchini Burundi mradi uliotekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa msaada wa serikali ya Japan umesaidia wakazi wa eneo la Cibitoke nchini Cibitoke siyo tu kuondokana na unywaji wa maji machafu  yenye wadudu, bali pia kuepusha watoto dhidi ya magonjwa na watoto wa shule kuondokana na zahma ya kutembea muda mrefu kwenda kuteka maji badala ya kwenda shuleni.

Video iliyoandaliwa na UNICEF Burundi imeanza kwa kuonesha katikati ya vilima vya jimbo la Cibitoke, nchini Burundi mwanamke aitwaye Solange akionekana kuelekea kuteka maji akiwa na kumbukumbu za siku za awali za maji yasiyo safi na salama.  

Solange anasema, "tulilazimika kutembea umbali mrefu kusaka maji, kuna wakati naondoka nyumbani saa 7 mchana na ninarejea saa 10 jioni."

Umbali uliwalazimu kuteka maji ya mtoni, lakini nayo hayakuwa safi na salama kwani anasema kuna wakati ukipikia ugali, ukitafuna unakutana na wadudu. 

UNICEF Burundi inasema asilimia 39 ya watoto nchini humo hawapati maji safi na salama. 

Solange anasema hilo lilisababisha kila mara wapeleke watoto wao hospitali kwa kuwa walikuwa wanaugua kwa kunywa maji machafu. 

Mradi wa ujenzi wa vituo vya maji safi mjini Cibitoke kwa msaada wa Japan ukawa mkombozi kwa kaya 2,000.

Solange anasema "leo hii faida ni kwamba maambukizi ya magonjwa yamepungua, zamani tulipokunywa maji ya mto Nyembeshage, tulikwenda kwa daktari mara tatu kwa mwezi, lakini sasa inaweza kupita miezi miwili bila kwenda kwa daktari." 

Mireille, mtoto mwanafunzi huyu anasema zamani maji yalikuwa mbali, alichelewa sana kufika shuleni, alama zangu zilikuwa mbayá, lakini sasa ni dakika moja tu kwenda kuteka maji, sasa tuna furaha.