Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande kinzani Yemen acheni kushambulia miundombinu ya maji- UNICEF

Hapa ni Hudaidah nchini Yemen ambako mama na watoto wake wakisubiri msaada kwenye kituo cha dharura kinachopata usaidizi kutoka UNICEF
UNICEF
Hapa ni Hudaidah nchini Yemen ambako mama na watoto wake wakisubiri msaada kwenye kituo cha dharura kinachopata usaidizi kutoka UNICEF

Pande kinzani Yemen acheni kushambulia miundombinu ya maji- UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetaka pande kinzani kwenye mzozo nchini Yemen ziache mara moja mashambulizi dhidi ya miundombinu ya maji ya kunywa.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta H. Fore amesema hayo leo kupitia taarifa iliiyotolewa huko Sana’a Yemen na New York, Marekani.

Amesema “mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia na huduma za binadamu hayakubaliki, ni kinyume na utu na pia yanakiuka sheria za msingi za vita na kwamba ghasia zinazoendelea na mashambulizi ya mara kwa mara ya miundombinu ya kiraia huko Hudaidah ni tishio la moja kwa moja la uhai wa mamia ya maelfu ya watoto na familia zao.”

Bi. Fore amesema licha ya kutambua hivyo, katika siku chache zilizopita kumekuwepo na msururu wa mashambulizi dhidi ya mifumo hiyo muhimu kwa uhai wa watoto na familia zao.

Ametolea mfano bohari ya UNICEF inayohifadhi misaada ya kibinadamu ikiwemo vifaa vya huduma za maji safi na kujifasi akisema ilishambuliwa kwa makombora mawili.

Uchotaji maji katika daraja lililobolewa kwa mashambulizi Yemen. OCHA linasaidia watu walio katika hali kama hiyo 2017
Picha ya OCHA/Giles Clarke
Uchotaji maji katika daraja lililobolewa kwa mashambulizi Yemen. OCHA linasaidia watu walio katika hali kama hiyo 2017

“Tarehe 28 Julai kituo cha huduma za kujisafi kinachopata msaada kutoka UNICEF huko wilaya ya Zabid kilishambuliwa ambapo tanki la mafuta liliharibiwa kabisa,” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF.

Amesema Yemen tayari inakabiliwa na uhaba wa maji safi na salama ya kunywa hali ambayo inahusishwa na milipuko ya kipindupindu na kuhara na hivyo mashambulizi dhidi ya miundombinu ya maji inakwamisha juhudi za kuzuia milipuko zaidi ya magonjwa hayo.

Bi. Fore ametoa wito kwa pande husika kulinda raia na miundombinu ya huduma za kiraia akisema vita nchini  Yemen havina washindi na vinapora mustakhbali wa watoto.