Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC inachunguza iwapo kuna ugonjwa wa Ebola huko Kivu Kaskazini

Mhudumu wa afya akimchanja dhidi ya Ebola, mwanaume mjini Beni, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC. (Maktaba)
World Bank/Vincent Tremeau
Mhudumu wa afya akimchanja dhidi ya Ebola, mwanaume mjini Beni, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC. (Maktaba)

DRC inachunguza iwapo kuna ugonjwa wa Ebola huko Kivu Kaskazini

Afya

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC inachunguza mtu anayeshukiwa kufariki kutokana na ugonjwa Ebola huko katika jimbo la Kivu Kaskazini

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO Kanda ya Afrika huko Kongo Brazzaville imesema mamlaka za afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinachunguza tetesi hizo za mtu anayeshukiwa kuwa na virusi vya Ebola, katika jimbo la mashariki mwa nchi hiyo la Kivu Kaskazini.

Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Matibabu ya Thecountry (INRB) iko katika harakati za kupima sampuli ili kubaini ikiwa mgonjwa huyo aliambukizwa Ebola.

Anayeshukiwa ni mwanamke mwenye umri wa miaka 46 aliyefariki tarehe 15 Agosti 2022 huko Beni, mji ulioko Kivu Kaskazini. Mgonjwa huyo alipata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Beni, awali kwa ajili ya magonjwa mengine, lakini baadaye, ilionyesha dalili zinazoambatana na ugonjwa wa virusi vya Ebola.

"Wakati uchambuzi ukiendelea, WHO iko tayari kusaidia maafisa wa afya kuchunguza kisa hicho na kujiandaa kwa uwezekano wa kuzuka kwa Ebola," amesema Dkt. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika.

Dkt Moeti amesema wafanyakazi wa WHO wanafanya kazi na mamlaka za afya kutambua mtu yeyote ambaye aliwasiliana na mwanamke huyo aliyefariki na kufuatilia afya zao. 

WHO pia itafanya kazi ili kuhakikisha hatua zinazofaa za kuzuia na kudhibiti maambukizi zimewekwa, kwamba matibabu yanaweza kupatikana kwa wale wanaohitaji, na kuongeza ufahamu kuhusu Ebola miongoni mwa jamii za wenyeji.