Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Yemen, WHO yapeleka msaada wa vifaa vya matibabu

Wakimbizi wa ndani kwenye kambi jimboni Al-Dhale'e nchini Yemen
© UNOCHA/Mahmoud Fadel-YPN
Wakimbizi wa ndani kwenye kambi jimboni Al-Dhale'e nchini Yemen

Mafuriko Yemen, WHO yapeleka msaada wa vifaa vya matibabu

Afya

Katika kuchukua hatua za dharura kusaidia jamii zilizoathiriwa na mafuriko nchini Yemen, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limepeleka msaada wa dharura wa vifaa vya matibabu ikiwemo maabara kwa lengo la kuinua uwezo wa timu zinazotoa huduma za waathirika wa mafuriko waliopata kiwewe

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Sana’a Yemen inasema pamoja na kutoa vifaa hivyo, WHO inaungana kwenye kutoka huduma na mamlaka za afya za kitaifa na watoa huduma wa kibinadamu.
Misaada hiyo ya WHO ni pamoja na wataalamu wabobevu kwenye masuala ya kiwewe, magari 6 ya kubebea wagonjwa na imeunda vituo 34 vya kuchunguza magonjwa kwenye jimbo la Ma’rib ambalo ndio limeathirika zaidi.

Mafuriko hayo yakiwa yamechochewa na mvua kubwa za msimu, yamesambaratisha majimbo kadhaa ya Yemen tangu katikati ya mwezi uliopita, na hadi sasa zaidi ya kaya 35,000 kwenye wilaya 85 za majimbo 16 zimeathirika.

WHO inasema mafuriko hayo yamesababisha vifo vya takribani watu 77, wakiwemo watoto kwenye majimbo ya Al Bayda, Amran, Dhamar, Hajja, Ma’rib, na Sana’a.

Halikadhalika miundombinu muhimu kama ile ya maji, huduma za umma bila kusahau mali binafsi za watu, imeharibika.

WHO pia itapatia hospitali 11 kila mwezi lita zaidi ya 145,000 za mafuta.

Katika jimbo la Al Hodeidah, WHO imepatia maabara kuu  vifaa pamoja na kupatia mafunzo ya uchunguzi wa Malaria kwa wataalamu 25 wa maabara.

Mwakilishi wa WHO nchini Yemen, Dkt. Adham Rashad amesema, “hatari ya magonjwa yaenezwayo kwa maji na vimelea, ikiwemo Malaria, Kipindupindu na mengine inazidi kuwa kubwa, mvua kubwa zaidi inatarajiwa kuendelea hadi mwisho wa mwezi huu wa Agosti, tumeimarisha hatua zetu kufikia waathirika na kuzuia uwezekano wowote wa mlipuko wa magonjwa haya.”