Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia zaongezeka huko Gaza na Israel, Wapalestina 13 wafariki dunia

Mji wa Gaza
Ziad Taleb
Mji wa Gaza

Ghasia zaongezeka huko Gaza na Israel, Wapalestina 13 wafariki dunia

Amani na Usalama

Mratibu wa Misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi ya Palestina inayokabiliwa wa mabavu Lynn Hastings amesema ana wasiwasi Mkubwa kuhusu ongezeko la ghasia huko Gaza na Israel. 

Taarifa aliyoitoa hii leo kutoka Jerusalem Hastings amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la ghasia zinazoendelea ndani na karibu na Gaza kati ya wanamgambo wa Kipalestina na Israel.

“Ghasia hizo hadi sasa zimegharimu maisha ya Wapalestina 13 kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel, akiwemo mtoto wa miaka mitano na mwanamke mmoja. Ripoti zinaonyesha kuwa zaidi ya Wapalestina 100 wamejeruhiwa na Waisrael 7 kujeruhiwa.”

Maeneo ya makazi katika Gaza na Israel yameshambuliwa na nyumba kuharibiwa, familia 31 huko Gaza tayari zimeachwa bila makazi.”

Ameeleza hali ya kibinadamu huko Gaza tayari ni mbaya na kutokana na ghasia zinazoendelea inaweza kuwa mbaya.

“Uhasama huu lazima usitishwe ili kuepusha vifo na majeraha zaidi ya raia huko Gaza na Israel. Kanuni na sheria za kimataifa za kibinadamu zikiwemo zile za kuchukua tahadhari  na kuwa na uwiano lazima ziheshimiwe na pande zote.” Amesema mratibu huyo wa Misaada wa UN

Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) huko Gaza
Ziad Taleb
Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) huko Gaza

Mengine yanayozidisha hali mbaya

Mafuta yanayotumika katika kiwanda cha nishati cha Gaza yanatarajiwa kuisha hii leo, umeme tayari umekatika. Uendeshaji unaoendelea wa vifaa vya huduma za kimsingi kama vile hospitali, shule, maghala, na makazi maalum kwa wakimbizi wa ndani ni muhimu lakini sasa yako hatarini. 

Safari za kutoka sehemu moja kwenda nyingine na ufikiaji wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, kwa ajili ya shughuli muhimu za matibabu, na kufikisha bidhaa muhimu ikiwa ni pamoja na chakula na mafuta kwenda Gaza, hazipaswi kuzuiwa ili mahitaji ya kibinadamu yaweze kufikiwa.

“Mamlaka ya Israeli na makundi ya wapiganaji wa Palestina lazima waruhusu mara moja Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu kupeleka mafuta, chakula, na vifaa vya matibabu na kupeleka wafanyakazi wa kibinadamu kwa mujibu wa kanuni za kimataifa, hii inajumuisha hasa kuhakikisha ufikiaji na usalama kupitia vivuko muhimu vya mpaka. Tuko tayari kufanya kazi na pande zote ili kuhakikisha mahitaji ya kibinadamu yanatimizwa. “Ameeleza Hastings kwenye taarifa yake.

Pia amerudia ombi lilikotolewa na Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa pande zote la kukomesha kuongeza hali kuwa mbaya na kusitishwa kwa ghasia, ili kuepusha athari za uharibifu, hasa kwa raia.