Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naibu Mkuu wa OCHA Joyce Msuya ahitimisha ziara yake nchini Uturuki

Magari yaliyobeba misaada yakiwa kwenye foleni katika mpaka wa Uturuki kuingia Syria
OCHA/David Swanson
Magari yaliyobeba misaada yakiwa kwenye foleni katika mpaka wa Uturuki kuingia Syria

Naibu Mkuu wa OCHA Joyce Msuya ahitimisha ziara yake nchini Uturuki

Msaada wa Kibinadamu

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA Joyce Msuya amehitimisha ziara yake ya siku tano nchini Uturuki ambapo mbali na kufanya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo alikutana na kuzungumza na wakimbizi. 

Taarifa hiyo iliyotolewa na Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq wakati akizungumza na waandishi wa habari jijii New York, Marekani imeeleza Naibu Mkuu huyo wa OCHA akiwa Gaziantep na Hatay alikutana na wanawake wakimbizi wa Syria, wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wafadhili na mamlaka za serikali ya Uturuki zinazohusika na misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inayovuka mipaka.

“Msuya ameipongeza serikali ya Uturuki kwa kuunga mkono kazi za kibinadamu na kuishukuru kwa kuendelea kuhifadhi wakimbizi zaidi ya milioni 3.7” Haq amewaambia waaandishi wa habari. 

Ufikishaji misaada Syria 

Zaidi ya watu milioni 4.1 walioko kaskazini magharibi mwa Syria wanategemea misaada ya Umoja wa Mataifa ili kukidhi mahitaji yao ya kimsingi. 

“Kila mwezi tunapeleka chakula na misaada mingine kutoka Uturuki na inawafikia watu milioni 2.4 nchini Syria na tunatumaini kutakuwa na ongezeko la kufufua pamoja na miradi ya kujikimu kimaisha”

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa ruhusa ya upitishaji wa misaada ya kibinadamu kwenda nchini Syria ambayo imebaki miezi tisa kabla ya kuisha wakati wa msimu wa baridi iwapo Baraza hilo halitaongeza muda. 

“Wakati wa ziara yake katika kituo cha Umoja wa Mataifa cha usafirishaji wa mizigo huko Hatay Msuya aliona mchakato mkali wa ufuatiliaji unaoendelea katika mpaka na akasisitiza namna utaratibu huo unavyoleta mabadiliko ya kweli.” 

Haq amesema wakati juhudi zinaendelea ili kuongeza usafirishaji zaidi wa misaada kwenda nchini Syria, kwa sasa ufikishaji wa misaada Syria hauwezi kuongezeka kupitisha misaada zaidi katika mpaka wa Uturuki na Syria.