Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa utaweza kujipima mwenyewe VVU kwa dola 1  

Muuguzi akifanya vipimo vya VVU katika Hospitali ya Wau, Sudan Kusini
© UNICEF/Albert Gonzalez Farran
Muuguzi akifanya vipimo vya VVU katika Hospitali ya Wau, Sudan Kusini

Sasa utaweza kujipima mwenyewe VVU kwa dola 1  

Afya

Ushirikiano mpya uliotangazwa leo Julai 27 kati ya Clinton Health Access Initiative (CHAI) yaani mpango wa Clinton wa upatikaji Afya, MedAccess ambalo ni shirika linalolenga upatikanaji wa dawa kwa bei nafuu, na Kampuni ya Wondfo Biotech, utafanya uchunguzi wa Virusi Vya UKIMWI, VVU upatikane kwa dola 1 fedha za kimarekani kwa sekta ya umma katika nchi za kipato cha chini na cha kati, na hivyo kufanya kufanya kipimo hicho kuwa cha bei ya chini zaidi katika vipimo vyote vya kujipima VVU vilivyoidhinishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO. 

WHO inasema licha ya kuwepo kwa uchunguzi na matibabu ya bei nafuu, duniani kote kuna wastani wa watu milioni 5.9 wenye VVU ambao bado hawajui hali zao. Idadi kuu (ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara ya ngono, wanaume wanaofanya ngono na wanaume, watu waliobadili jinsia, watu wanaojidunga dawa za kulevya, watu walio katika magereza na maeneo mengine yaliyofungwa) na wapenzi wao ndio wanaochangia maambukizi mapya ya VVU, na wasichana na wanawake vijana uwezekano wa kupata VVU ni mara 3 zaidi kuliko wenzao wa kiume. Wengi, wakiwemo watu kutoka makundi muhimu na vijana, wanaona kujipima VVU kuwa chaguo rahisi na la siri. 

"Tangazo la bei mpya ni hatua muhimu ya kufanya upimaji wa VVU kwa ajili ya uchunguzi na ufuatiliaji wa kinga kupatikana duniani kote," amesema Dkt. Meg Doherty, Mkurugenzi wa WHO anayehusika na programu za VVU, Homa ya Ini au Hepatitis na Maaambukizi kwa njia ya ngono STI. "Itasaidia programu kutoa huduma ya kujipima VVU katika njia za utoaji wa huduma za umma, jamii na sekta binafsi." Ameongeza. 

WHO inapendekeza kujipima VVU kama njia salama, sahihi na madhubuti ya kuwafikia watu ambao huenda wasingepima, na hadi sasa, imeptishsha kwangazi za awali vipimo sita 6 vya kujipima binafsi VVU, kwa kutumia majimaji ya kinywa na damu, ili kuhakikisha ubora na matumizi ya vifaa hivi.  

"Vipimo vya uchunguzi ambavyo vimehakikiwa ubora ni muhimu kwa mifumo bora ya afya. Kuongezwa kwa kipimo kipya cha kujipima katika orodha ya Uchunguzi inachangia katika kuhakikisha upatikanaji wa vipimo salama, vinavyofaa na vya bei nafuu vya ubora mzuri.” Amesema Rogério Gaspar, Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti na Masharti ya Awali katika WHO. 

Ulimwenguni, nchi nyingi zimeunda sera za kitaifa zinazounga mkono kujipima VVU, na utekelezaji unakua kwa kasi. Kufikia Juni 2022, nchi 98 – asilimia 52 ya nchi zinazoripoti kwa WHO zina sera ya kujipima VVU, lakini utekelezaji uko nyuma, na ni nchi 52 pekee duniani zinazotekeleza mara kwa mara. WHO inakadiria kuwa wafadhili wakuu na serikali katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati katika mwaka wa 2021 zilinunua zaidi ya vifaa milioni 10 vya  kujipima VVU. Ingawa utabiri wa siku zijazo unaonekana kuwa mzuri, upatikanaji wa bidhaa za bei ya chini za kujipima ni muhimu kushughulikia hitaji kubwa la kujipima VVU. 

Wakati wa COVID-19, nchi nyingi zilihamia kuharakisha mbinu za kupima VVU ambazo zilijumuisha kujipima VVU. Upunguzaji wa bei mpya huu wa sasa ni fursa kwa programu zaidi kuchukua na kutoa kujipima VVU na kuleta huduma za upimaji, matibabu na kinga kwa wale wanaozihitaji zaidi. Huu ni wakati mwafaka, kwani WHO imetoa mwongozo mpya kuhusu utoaji wa huduma tofauti kwa ajili ya kuzuia kabla ya kuambukizwa (PrEP), unaojumuisha masharti ya kutumia vipimo vya VVU binafsi ili kuongeza upatikanaji na kuzuia maambukizi mapya.