Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia kushuhudia kudorora zaidi kwa uchumi: IMF

Mfanyabiashara barabarani akiuza chakula barani Afrika
IMF
Mfanyabiashara barabarani akiuza chakula barani Afrika

Dunia kushuhudia kudorora zaidi kwa uchumi: IMF

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti ya hali ya uchumi kwa robo ya pili ya mwaka huu wa 2022 ambao ni mwezi Aprili hadi Juni ambayo imetolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF imesema matarajio ya ukuaji wa uchumi duniani yanazidi kukumbwa na kiza na yanakosa uhakika na kwamba matumaini ya uchumi kukwamuka mwaka 2021 yanazidi kuyoyoma mwaka huu wa 2022. 

“Mtazamo umekuwa giza sana tangu mwezi Aprili.” Ni Pierre-Olivier Gourincha Mkurugenzi wa Idara ya utafiti wa IMF akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya IMF jijini Washington DC nchini Marekani ambapo ameeleza hali ya kiuchumi inazidi kuwa mbaya. 

Anasema “Ulimwengu hivi karibuni unaweza kushuhudia kudorora kunakopeleka uchumi wa kimataifa ukingoni  ikiwa ni miaka miwili tu baada ya kushuhudia mdodoro wa mwisho.”

IMF imetaja sababu kuu za kudorora kwa uchumi kuwa ni kupanda kwa mfumuko wa bei, kupanda kwa viwango vya riba, thamani ya juu ya dola ya kimarekani, athari za vita vya Ukraine na kushuka kwa ukuaji wa nchi ya China.

Mkuu huyu wa idara ya Utafiti amesema kinachohitajika sasa ni ushirikiano wa pande nyingi katika maeneo mengi ilikupunguza hatari ya dunia kugawanyika na kuimarisha ushirikiano kwakuwa hiyo ndio njia bora ya kuboresha matarajio ya kiuchumi kwa wote na kupunguza hatari ya kugawanyika kwa kijiografia.

Mfumuko wa bei duniani umerekebishwa na unatarajiwa kubaki juu kwa muda mrefu zaidi.
IMF/World Economic Outlook
Mfumuko wa bei duniani umerekebishwa na unatarajiwa kubaki juu kwa muda mrefu zaidi.

Gourincha amesema “Kilicho muhimu sana hapa ni kwamba katika hali fulani kuna kipaumbele kimoja kikubwa katika hatua hii, na ni kurudisha utulivu wa bei katika uchumi wa juu na katika masoko yanayoibukia pia, kwakuwa wengi kwasasa wameona shinikizo la bei kuwa juu. “

IMF imesema mfumuko wa bei unaoendelea nchini Marekani na mataifa mengine makubwa ya kiuchumi unasababisha benki kuu kuongeza viwango vya riba. Wakati huo huo, kuna hoja ya usalama wa dola ya marekani ikimaanisha kuwa masoko yanayoibukia hasa yanakabiliwa na bei ya juu huku pia gharama ya kulipa deni ikiongezeka. 

Kishawishi kwa sasa kitakuwa nchi kusukuma mageuzi ya kiuchumi au kuongeza matumizi, lakini IMF imeonya kuwa hatua hiyo  kwasasa itaongeza maumivu zaidi baadaye.