Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP Tanzania yajenga stadi za kilimo bora kwa vijana Kilimanjaro

WAnafunzi kutoka Chuo cha Ufundi stadi cha Kibosho nchini Tanzania wakijfunza mbinu za kilimo cha kupanda mazao kwenye maji bila udongo ikiwa ni mafunzo kwa msaada wa UNDP.
UNDP Tanzania
WAnafunzi kutoka Chuo cha Ufundi stadi cha Kibosho nchini Tanzania wakijfunza mbinu za kilimo cha kupanda mazao kwenye maji bila udongo ikiwa ni mafunzo kwa msaada wa UNDP.

UNDP Tanzania yajenga stadi za kilimo bora kwa vijana Kilimanjaro

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP nchini Tanzania limetekeleza kwa vitendo wito wa Umoja wa MAtaifa wa kutaka vijana kupatiwa stadi za msingi nje ya darasani kama njia mojawapo ya kuwawezesha  kumudu kazi za siku za usoni.

 

UNDP Tanzania limetekeleza mradi wa kujenga stadi za vijana kupitia Chuo Cha Mafunzo stadi za Kibosho, KiVTC mkoani Kilimanjaro ambako vijana wanapata stadi za kilimo cha kisasa halikadhalika ufugaji bora, stadi ambazo pia wanazipeleka kwa jamii na wazazi wao.

Kilimo bila kutumia udongo

Mkuu wa Chuo hicho, Daniel Mboya, anasema miongoni mwa stadi ni kilimo cha majani ya kulisha mifugo, kilimo ambacho kinatumia maji na virutubisho vingine vyote isipokuwa udongo, kwa kiingereza Hydroponic Fodder.

Kwenye shamba la chuo hicho, makasha yaliyoota majani hayo ya kulisha mifumo yamestawi na hakuna udongo isipokuwa maji na virutubisho.

Bwana Mboya anasema kilimo hiki, “inatusaidia sisi kwenye kilimo kwani ufugaji tunaofanya hapa shuleni tumepunguza gharama za ufugaji kwani hayo majani yanalisha mifugo yetu, na mifugo inatupatia mazao mengine kama vile mbolea na maziwa.”

UNDP pia imesaidia chuo hicho kwenye kilimo cha mboga na matunda kupitia Chama cha wakulima wa mboga na matunda Tanzania, TAHA.
Wanafunzi wanapeleka ujuzi kwa wazazi na jamii

“Wanafunzi wetu wengi wanatoka tarafa ya Kibosho, kwa hiyo nao wanatumika kwenda kutoa mafunzo pia kwa wazazi wao na vikundi vilivyoko huko kwao,” amefafanua Bwana Mboya.

Amesema stadi wanazofundishwa vijana zinalenga kuwawezesha kujitegemea baada ya mafunzo. 

Mafunzo pia kuongezea mazao thamani

Mradi wa UNDP pia unapatia vijana stadi za kuongezea thamani mazao, “ni kipengele ambacho wanafunzi na wanajamii wamekipenda zaidi. Tunawafundisha namna ya kukausha, kufungasha mazao. Mfano kutengeneza unga. Na pia kuna siku za wakulima kutembelea mashamba au miradi yetu na kujifunza,” amefafanua Bwana Mboya huku akisema, “wameleta thamani kwenye maisha ya wanafunzi na jamii yetu.”

Kwa mujibu wa UNDP, matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo kama vile umwagiliaji na mashine za kuvunia, huongeza thamani kwenye mavuno na hatimaye wakulima kuuza mazao yao na kujipatia kipato.