Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msimu wa baridi kali zaidi tangu uhuru waja Ukraine, OCHA na wadau wajipanga

Nchini Ukraine, muhudmu wa afya akipishana na watu wanaokatiza eneo linalosimamiwa na serikali. (Maktaba)
UNOCHA/Lizaveta Zhuk
Nchini Ukraine, muhudmu wa afya akipishana na watu wanaokatiza eneo linalosimamiwa na serikali. (Maktaba)

Msimu wa baridi kali zaidi tangu uhuru waja Ukraine, OCHA na wadau wajipanga

Msaada wa Kibinadamu

Takriban raia wa Ukraine milioni 15.7 wanahitaji msaada wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na wakimbizi wa ndani milioni 7.1 (IDPs) wanaoishi katika nyumba za kibinafsi na vituo vya pamoja, imeeleza taarifa ya leo ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA. 

Baridi kali zaidi tangu uhuru 

OCHA inaeleza kuwa mamilioni ya watu wa Ukraine wanaishi katika nyumba zilizoharibiwa, au katika majengo ambayo hayafai vizuri kutoa ulinzi wa kutosha dhidi ya hali mbaya ya msimu wa baridi. Kwa kutazamia uwezekano wa "msimu wa baridi mbaya zaidi tangu uhuru wa Ukraine", fedha za ziada zinahitajika haraka ili kuandaa jamii zilizo katika hatari na kufuatilia kwa haraka shughuli za dharura ambazo zitakuwa na matokeo bora zaidi kwa watu binafsi na familia zilizo katika mazingira magumu. Huku halijoto ya msimu wa baridi ikitabiriwa kushuka hadi nyuzi joto -20 Selsiasi katika sehemu fulani za nchi, athari kali itahisiwa na mamilioni ya watu wanaoishi katika hali ya chini ya kiwango au bila vikinga baridi vya kutosha vya kibinafsi au upatikanaji wa mfumo joto. 

“Mipango ya mapema ni muhimu ili kuhakikisha hali ya maisha ya joto, salama na yenye hadhi kwa watu walioathirika kabla ya kuanza kwa majira ya baridi,” imesema OCHA ikiongeza kuwa, “Serikali ya Ukraine inaongoza katika utayarishaji na utekelezaji wa shughuli za uwekaji mipango ya majira ya baridi kali, huku Umoja wa Mataifa na wadau wa kibinadamu wakishirikiana ili kukamilisha hili kupitia hatua za kushughulikia mahitaji makubwa ya kibinadamu katika kipindi cha majira ya baridi kali.”  

Kwa maandalizi ya kutosha na ufadhili wa wakati unaofaa, wakati wa miezi ya baridi kali maisha mengi yanaweza kuokolewa, hasa wale walio katika mazingira hatarishi waliofurushwa na kuathiriwa na vita. 

Mpango huu umejikita katika uzingatiaji watu, ukitoa kipaumbele kwa wakimbizi wa ndani na watu wanaoishi katika makazi ya chini ya kiwango na hatua muhimu ambazo zinaweza kuhakikisha hali ya maisha ya joto, salama na yenye hadhi inayokamilishwa na shughuli za kisekta zinazolengwa.  

Kwa msingi huo mpango huo wa OCHA unatoa wito wa dola milioni 226 kuanza ununuzi, usambazaji na wakati muhimu, shughuli za ukarabati, zinazowapa watu milioni 1.7 msaada wa awali kabla ya msimu wa baridi wa mwaka 2022/2023.