Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Familia 3 kati ya 10 hazina uhakika wa kupata chakula nchini Sri Lanka

Sri Lank inakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na hali mbaya ya kiuchumi
© WFP/Josh Estey
Sri Lank inakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na hali mbaya ya kiuchumi

Familia 3 kati ya 10 hazina uhakika wa kupata chakula nchini Sri Lanka

Msaada wa Kibinadamu

Familia 3 kati ya 10 sawa na watu milioni 6.26 nchini Sri Lanka hazina uhakika wa kupata chakula na pindi kinapopatikana hakina lishe kamili na ndio maana shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limepanga kufikishia msaada wa chakula watu milioni 3 walio katika katika maeneo mbalimbali sambamba na kugawa mlo shuleni. 

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo imeeleza kuwa familia nyingi zinaendelea kuathirika na hali mbaya ya kiuchumi na ukosefu wa chakula wakati ambapo mfumuko wa bei nchini humo umefikia asilimia 57.4 kwa taarifa za mwezi Juni mwaka huu 2022.

Msaada huo wa WFP kwa watu milioni 3 utawapatia chakula cha dharura, lishe Pamoja na mlo shuleni kwa wanafunzi kuanzia sasa mpaka mwezi Desemba 2022.

WFP pia imesambaza vocha 2,100 sawa na asilimia 88 ya vocha zinazohitajika kwa wanawake wajawazito.

Familia zinazoishi vijijini nchini Sri Lanka zinahakaka kusaka mlo wa siku
© WFP/Josh Estey
Familia zinazoishi vijijini nchini Sri Lanka zinahakaka kusaka mlo wa siku

Mbinu mbadala

Asilimia 61 ya familia zilizohakikiwa na WFP zimebuni njia mbalimbali za kujipatia chakula ikiwa ni Pamoja na kupunguza kiwango cha chakula wanachokula katika kaya.

Hata hivyo uhakiki huo umegundua familia mbili kati ya tano hazili chakula chenye lishe kamili.

Hali ni mbaya zaidi miongoni mwa watu wanaoishi katika mashamba makubwa ya kilimo ambapo nusu ya kaya hazina chakula. Kaya hizo zina hali duni ilikinganisha na watu wengine wanaoishi mijini na vijijini.

Familia 200,000 zinatumia mbinu za dharura za kujikimu ambazo hata hivyo zitakuwa na athari kubwa za kiuchumi kwao katika kipindi cha kati na muda mrefu mathalan watashindwa kupata fedha kwa ajili ya kununua chakula kwakuwa kaya nyingi kwa sasa zinategemea kukopa fedha ili waweze kununua chakula na mahitaji mengine muhimu.

Sri Lanka inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta huku taifa hilo likikumbwa na msukosuko wa kiuchumi.
WFP/Josh Estey
Sri Lanka inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta huku taifa hilo likikumbwa na msukosuko wa kiuchumi.

Watu wengi zaidi kuathirika

WFP inakadiria kuwa watu wengi zaidi watadumbukia kwenye njia hii ya kujikimu ya kupunguza mlo wakati huu ambapo hali inazidi kuwa mbaya.

Shule na ofisi za serikali zimefungwa kutokana na uhaba wa usambazaji wa mafuta mpaka hapo watakapo taarifiwa zaidi.

Sekta za kilimo, afya na Maisha ndio zilizoathirika zaidi na mfumuko huu wa bei ambao haujawahi kushuhudiwa tangu mwaka 1954.