Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria kudhibiti ukiukwaji wa haki za binadamu na mazingira ufanywao na kampuni za biashara ni muhimu – Mtaalamu

Mtoto wa kike akiwa ameketi juu ya ukuta ndani ya kiwanda cha gundi ambako wafanyakazi wanachakata taka za ngozi ili kupata gundi. Hapa ni Hazaribagh karibu na mto Buriganga kwenye mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka.
UNICEF/Noorani
Mtoto wa kike akiwa ameketi juu ya ukuta ndani ya kiwanda cha gundi ambako wafanyakazi wanachakata taka za ngozi ili kupata gundi. Hapa ni Hazaribagh karibu na mto Buriganga kwenye mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka.

Sheria kudhibiti ukiukwaji wa haki za binadamu na mazingira ufanywao na kampuni za biashara ni muhimu – Mtaalamu

Tabianchi na mazingira

Ukataji holela wa misitu, uzalishaji wa kemikali na plastiki Pamoja na uchimbaji wa mafuta kisukuku sambamba na shughuli zingine zinazofanywa na kampuni za kibiashara vinadhuru siyo tu binadamu bali pia sayari dunia, ameonya  hii leo mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu na mazingira.

Kupitia taarifa iliyotolewa hii leo jijini Geneva, Uswisi na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR, mtaalamu huyo David Boyd amesema, “kampuni za kibiashara zinazoendesha shughuli zao kiuchumi duniani, zinakiuka haki za kuwa na mazingira safi, yenye afya na endelevu pamoja na haki za binadamu.”

Wenye haki hupuuzwa na wakisaka hukumbwa na vitisho

Bwana Boyd amesema ukiukaji wa haki za binadamu na za mazingira unaofanywa na kampuni za biashara umesambaa huku hatua thabiti za wale wenye haki zao zikiyoyoma.
 
“Wenye haki mara nyingi hawapati majawabu,” ametanabaisha mtaalamu huyo akisema, “wale ambao haki zao zinazingatiwa inawabidi wahangaike wakikumbana na vikwazo vya kisheria, kifedha na vinginevyo vingi. Mara nyingi wanapata vitisho, wananyanyaswa na wanakumbwa na visasi kama siyo wao basi familia zao au jamii zao,” amesema Bwana Boyd.

Amefafanua kuwa wale wenye haki ambao mara nyingi huathiriwa na shughuli za kibiashara ni Watoto, wanawake, watu wa jamii ya asili, watu wenye asili ya Afrika, jamii za wenyeji, wakulima na watu wenye ulemavu.

“Wale ambao utambulisho wao unatoka katika makundi tofauti tofauti yaliyo hatarini zaidi, mathalani mwanamke na pia ana ulemavu, hukumbwa na vikwao zaidi katika kusaka haki,” amesema Bwana Boyd.

Uhiari kwa sekta ya biashara kulinda mazingira una changamoto

Kwa kuona hilo, mtaalamu huyo amependekeza kanuni na sheria za kudhibiti uvunjaji na ukiukwaji wa haki za mazingira na za kibinadamu unaofanywa na kampuni za kibiashara kwa kuzingatia kuwa, “kitendo cha mtu binafsi au kampuni ya kibiashara kuchukua hatua za kuzingatia haki kwa hiari, hazitoshelezi.”

Amesema kuna makubaliano ya kwamba sheria za kibinadamu na mazingira zinapaswa kuwajibisha kampuni za biashara kwa hatua zao zinazoathiri mazingira na binadamu.

Na zaidi ya yote, sheria kadhaa ziko mbioni kutungwa katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa, hatua ambazo zinatoa fursa ya kusongesha kanuni za Pamoja za kuwajibisha wafanyabiashara.

Kuna fursa mpya sasa

Ametolea mfano Kamisheni ya Ulaya ambayo imetoa pendekezo la mwongozo wa kanuni za kuzingatiwa na sekta ya biashara.

Halikadhalika Kanuni zinazoandaliwa na Umoja wa Mataifa zitakazokuwa na nguvu kisheria katika kusimamia haki za binadamu na shughuli za kampuni za kibiashara, kanuni ambazo zinatarajiwa kusongeshwa mwaka huu wa 2022.

 “Licha ya kasoro zake, kanuni hizo za Umoja wa Mataifa zikipitishwa zitakuwa ni Mkataba wa Kwanza wenye nguvu kisheria,” amesema Bwana Boyd.

Mapendekezo ya Bwana Boyd yana malengo yanayotegemeana na kanuni 10 za kisheria.

“Iwapo itapitishwa, mapendekezo hayo yataimarisha sheria za kuzuia ukiukwaji wa haki za binadamu na mazingira na usimamizi bora wa sekta ya biashara, na zaidi ya yote kuponesha majeraha kule ambako yanatokea.