Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila uvuvi endelevu, hatutatokomeza njaa na umaskini-FAO 

Samaki ambao ndio kwanza wametoka kuvuliwa katika eneo la santa Rosa de Salinas, Ecuador
FAO/Camilo Pareja
Samaki ambao ndio kwanza wametoka kuvuliwa katika eneo la santa Rosa de Salinas, Ecuador

Bila uvuvi endelevu, hatutatokomeza njaa na umaskini-FAO 

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linasema uvuvi uko njiapanda hususani katika nchi maskini ingawa ni wazi kuwa samaki ni muhimu katika kupambana na umaskini.

 

FAO inaeleza wasiwasi wake kuhusu uvuvi duniani kuwa ijapokuwa samaki ni muhimu kwa ajili ya chakula, lishe na ustawi wa maisha katika nchi nyingi maskini duniani lakini kuna mashaka kuhusu uendeleaji wake huku makadirio yakionesha kuwa asilimia 95 ya wavuvi wote wanaishi barani Afrika na Asia. 

“Bila uvuvi endelevu, hatutatokomeza njaa na umaskini.” Inaonya FAO. 

FAO inaeleza kuwa kwa sasa uvuvi uko njiapanda ingawa unajitahidi kuweka usawa kati ya uhakika wa chakula na uhifadhi wa bioanuwai na shirika hili linaona kuwa uvuvi endelevu ndilo jibu lakini changamoto iko katika kulifikia lengo ili vyote viwili yaani chakula na utunzanji bioanuai vipatikane.  

Hivi sasa FAO inafanya uchambuzi na ufuatiliaji wa hali ya kiasi cha samaki ulimwenguni. Kutokana na uchafuzi, mabadiliko ya hali ya hewa, uharibifu wa makazi  ya samaki na uvuvi uliopitiliza, idadi ya samaki katika viwango endelevu vya kibaolojia imeshuhudia kupungua kwa kiasi kikubwa.  

Aidha FAO inasema shida kubwa ni ugumu wa kisiasa wa kusimamia uvuvi katika hali ya viwango vya juu ya umasikini. Kuboresha uendelevu wa uvuvi kunategemea katika kuelewa ukweli wa ikolojia, kijamii na uchumi wa jamii husika.  

“Samaki na mazao ya samaki ni moja ya bidhaa zinazouzwa zaidi kimataifa,” zinaeleza takwimu za FAO zikiongeza kuwa katika nchi zinazoendelea, kipato kinachotokana na samaki ni kikubwa kuliko kipato chote cha bidhaa za kilimo. 

Ushauri wa FAO ni kwamba ili kupambana na vikwazo vyote vinavyozuia uvuvi endelevu kama vile uvuvi haramu na uvuvi usiodhibitiwa, ni muhimu kushirikisha jamii ambazo zinaathiriwa na hatua zitakazochukuliwa, na kwa kushirikiana, ulimwengu unaweza kufikia uvuvi endelevu katika karne hii ya 21 na hata zaidi.