Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pole wananchi na serikali ya Nigeria kwa shambulizi la 5 Juni- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Pole wananchi na serikali ya Nigeria kwa shambulizi la 5 Juni- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la kikatili kwenye kanisa katoliki la Mtakatifu Francis  huko Owo jimboni Ondo nchini Nigeria, shamaulio lililofanywa jana Jumapili na kusababisha vifo na majeruhi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, watu wenye silaha walifyatulia risasi waumini huku wakilipua vilipuzi kwenye kanisa hilo lililoko kusini-magharibi mwa Nigeria ambapo takribani watu 50 waliuawa, wakiwemo watoto na wengine kadhaa walijreuhiwa.

Mashuhuda wanasema watu  hao walivamia kanisa hilo wakati ibada inakaribia kumalizika na pamoja na kuua na kujeruhi, walimteka nyara padre aliyekuwa anaongoza ibada hiyo ya Pentekoste.
  
Katibu Mkuu kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wake, amesisitiza, “mashambulizi dhidi ya maeneo ya ibada yanachukiza. Nasihi mamlaka za Nigeria zifanye jitihada zote kuwafikisha mbele ya sheria watekelezaji wa shambuli hilo.”
  
Bwana Guterres pia ametuma salamu za rambirambi kwa wananchi na serikali ya Nigeria pamoja na familia za wafiwa huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Halikadhalika ameeleza mshikamano na wananchi na serikali ya Nigeria.