Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusikubali kuteseka kwa watoto Mali kuwe kitu cha kawaida -UNICEF

Mshauri wa mashinani kutoka UNICEF huko jimboni Kayes nchini Mali  akimweleza mama umuhimu wa kumpatia chanjo mwanae. (Machi 2019)
UNICEF/Seyba Keïta
Mshauri wa mashinani kutoka UNICEF huko jimboni Kayes nchini Mali akimweleza mama umuhimu wa kumpatia chanjo mwanae. (Machi 2019)

Tusikubali kuteseka kwa watoto Mali kuwe kitu cha kawaida -UNICEF

Amani na Usalama

Kumekuwa na ongezeko la visa vya ukatili dhidi ya watoto nchini Mali mwaka huu wa 2019 hususan mauaji na kuwakata viungo vya mwili, limesema  hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,UNICE na wadau. Arnold Kayanda na maelezo zaidi.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mijini Bamako, Mali, Dakar, Senegal, Geneva Uswisi na New York, Marekani, inanukuu taarifa za awali za Umoja wa Mataifa zikionesha kuwa watoto 150 waliuawa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2019 na wengine 75 walijeruhiwa katika mashambulizi ya kikatili. 

Aidha uandikishaji na utumikishwaji wa watoto katika vikundi vilivyojihami uliongezeka maradufu ikilinganishwa na wakati kama huo mwaka 2018, na zaidi ya shule 900 bado zimefungwa kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amesema, “wakati ukatili ukiendelea kusambaa nchini Mali, watoto wako hatarini zaidi ya kuuawa, kukatwa viungo na kuandikishwa jeshini.” 

Bi Fore amenukuliwa akisema kwamba, “tusikubali kuteseka kwa watoto kuwa kitu cha kawaida, ni lazima pande zote wasitishe mashambulio dhidi ya watoto na kuchukua hatua zinazohitajika kuwaepusha na hatari yoyote kwa mujibu wa sheria za kimataifa za sheria za kibinadamu. Watoto wanapaswa kuwa wakienda shule na kucheza na marafiki zao, lakini sio kuwa na wasiwasi kuhusu kushambuliwa au kulazimishwa kupigana.”

Ongezeko la vitendo vya ukatili, limeongeza pia mahitaji ya ulinzi kaskazini na katikati mwa Mali. 

Umoja wa Mataifa unasema katika eneo la Mopti, ongezeko la uhasama wa jamii na uwepo wa makundi yaliyojihami umesababisha mashambulio ya mara kwa mara ambayo yamesababihsa kuuawa na kukatwa viungo kwa watoto, kufurushwa na kuondokana na familia zao na kuwa hatarini ya ukatili wa kingono na kiwewe.Takriban watoto 377,000 wanakadiriwa kuhitaji msaada nchini Mali.

UNICEF imekuwa ikifanya kazi na mamlaka mashinani na wadau kuwasilisha huduma ya kiafya na kisaikolojia kwa watoto waliothirika na mzozo kwa ajili ya kusaidia kuwachiwa na kujumuihswa tena kwenye jamii waototo kutoka makundi yaliyojihami na kutoa huduma kwa manusura wa ukatili ikiwmeo ukatli wa kingono. Mwaka huu wa 2019, UNICEF inalenfa kutoa msaada wa kisaikolojia kwa watoto 92,000 wa kike na kiume.

Mzozo wa Mali unasalia kuwa moja ya mizozo iliyofadhiliwa kwa kiasi kidogo duniani. Kuanzia 2016 hadi 2018, programu ya ulinzi wa dharura wa UNICEF nchini Mali ulifadhiliwa kwa asilimia 26 tu. Mwaka 2019, UNICEF inatoa ombi la dola milioni 4 kufikia mahitaji ya ulinzi wa watoto na wanawake nchini Mali.