Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku 100 za uvamizi wa Urusi nchini Ukraine: Vita ikome sasa- Guterres

Jengo la makazi ya watu likiteketea kwa moto baada ya kupigwa kombora kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv. Watu wawili walikufa na wengine 50 waliokolewa na wafanyakazi wa uokozi.
© UNDP Ukraine/Pavlo Petrov
Jengo la makazi ya watu likiteketea kwa moto baada ya kupigwa kombora kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv. Watu wawili walikufa na wengine 50 waliokolewa na wafanyakazi wa uokozi.

Siku 100 za uvamizi wa Urusi nchini Ukraine: Vita ikome sasa- Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa yake hii leo jijini New York, Marekani kuhusu siku 100 za uvamizi wa Urusi huko Ukraine,  akisema kuwa vita hiyo tayari imesababisha vifo vya maelfu ya watu, uharibifu wa kupita kipimo, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu usioelezeka na kuibua janga la pande tatu duniani: nishati, chakula na fedha, waathirikao zaidi ni watu walio hatarini, nchi na uchumi.

“Tangu kuanza kwa vita, Umoja wa Mataifa umekuwepo hima kusaidia watu wa Ukraine kukabiliana na madhara ya kibinadamu yatokanayo na vita hiyo, huku ukipazia sauti htari na madhara ya muda mrefu ya kuendelea kwa vita hivyo kwa taifa hilo, ukanda wa Ulaya na dunia nzima,” amesema Guterres.

Ni kwa mantiki hiyo amesema, “tunapotimiza siku 100 ya janga hili, narejelea wito wangu wa kukoma mara moja kwa ghasia, kuondolewa kwa vikwazo vya kufikisha misaada ya kibinadmu na kuhamisha kwa usalama raia walionasa maeneo yenye mzozo.”
Amesema Umoja wa Mataifa umejizatiti na harakati za kiutu, “lakini kama nilivyosisitiza mwanzoni,kutatua mzozo huu kunahitaji mashauriano na mazungumzo. Kadri pande husika zitakapozungumza haraka na kwa nia njema kumaliza vita hii, ndiyo itakuwa bora kwa Ukraine na Urusi na kwa dunia nzima.

 

Wakimbizi wa Ukraine waliowasili kituo cha treni cha Rzeszow nchini Poland.
© UNHCR/Maciej Moskwa
Wakimbizi wa Ukraine waliowasili kituo cha treni cha Rzeszow nchini Poland.

Wakati huo huo, Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu janga linaloendelea nchini Ukraine, Amin Awad amesema dunia hivi sasa haiko katika hali nzuri kutokana na vita vinavyoendelea nchini Ukraine vilivyosababishwa na uvamizi wa Urusi siku 100 zilizopita na hivyo kila hatua inapaswa kuchukuliwa vita hiyo ikome.

Ametoa kauli hiyo akihojiwa na Idhaa ya kiarabu ya Umoja wa Mataifa wakati huu ambapo vita hiyo imesababisha mfumuko wa bei za bidhaa duniani, mnyororo wa usafirishaji wa bidhaa umevurugika, maelfu ya watu wamekufa huku mamilioni wakiwa wamekimbia makazi yao bila kusahau uharibifu wa miundombinu ya kiraia kama vile shule na hospitali.

Kuna nuru lakini vita imevuruga dunia

“Kuna matumaini kuwa vita hii itaisha. Na katika muktadha huo, hili haliwezi kufanywa na Urusi au Ukraine peke yake. Vikwazo ni vikali kwa Urusi, maisha ya watu yamepotea, hospitali, shule, makazi,m vituo vya reli, nishati na usafirishaji vimeharibiwa. Ni uharibifu mkubwa kwa dunia,” amesema Bwana Awad.
Ni uharibifu mkubwa kwa dunia kwa sababu, “Ukraine inachangia takribani asilimia 15 hadi 20 ya chakula kinachohitajika duniani. Chakula hiki sasa kimenasa Ukraine, na siku chache zijazo msimu mpya wa mavuno unaanza; kuna mvurugano wa usambazaji wa chakula.”

Mvulana wa miaka 10 akitembea mbele ya jengo lao katikati mwa Chernihiv, Ukraine lilioharibiwa na shambulizi la anga.
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Mvulana wa miaka 10 akitembea mbele ya jengo lao katikati mwa Chernihiv, Ukraine lilioharibiwa na shambulizi la anga.

Watoto wamenitia machungu

Alipoulizwa taswira iliyosalia zaidi kichwani mwake baada ya kuwepo Ukraine kwa miezi kadhaa na kushuhudia kiwango cha uharibifu, Bwana Awad amesema mambo ni mengi lakini kubwa zaidi, “simulizi zilizobakia kwenye fikra zangu ni pale nilipozuru kwa gari baadhi ya maeneo yenye uharibifu na kuona watoto waliokimbia makazi yao na sasa wako peke yao barabarani bila wazazi au walezi na hawana pa kwenda. Nadhani hili ni gumu zaidi na ni moja ya taswira mbaya zaidi za vita na vita hii lazima ikome.”

Raia ndio wanalipa gharama kubwa zaidi

Bwana Awad amesema siku hizi 100 za uvamizi wa Urusi nchini Ukraine zimegharimu zaidi raia. “Ni hali ya kukata tamaa. Kuna takribani wakimbizi wa ndani milioni 8 nchini Ukraine na wengine milioni 6 wamekimbilia nchi Jirani. Takribani milioni 15 hawakuondoka majumbani mwao lakini wameathirika na kupotea kwa mbinu za kujipatia kipato.”

Amesema hawana huduma kama vile elimu, afya na nyinginezo na mamilioni ya watoto hawaendi shuleni.

Mfumo wa hifadhi ya jamii umezidiwa uwezo. Huduma za serikali halikadhalika.”Kwa kweli hali ya kibinadamu nayo ni mbaya. Hali ni mbaya sana,” amesema Mratibu huyo wa UN kwa janga la Ukraine.

Amin Awad, (kushoto) akiwa kwenye mazungumzo na maafisa wa serikali ya Ukraine yenye lengo la kufanikisha usambazaji wa misaada ya kibinadamu. (mkutano ulifanyika mwezi Aprili)
Amin Awad
Amin Awad, (kushoto) akiwa kwenye mazungumzo na maafisa wa serikali ya Ukraine yenye lengo la kufanikisha usambazaji wa misaada ya kibinadamu. (mkutano ulifanyika mwezi Aprili)

Hatujapokea ombi la operesheni kama ya Mariupol

Alipoulizwa iwapo kuna operesheni nyingine kama ile iliyofanyika Mariupol ya kuhamisha raia kutoka eneo liliolokuwa na mapigano makali kama kule kwenye mtambo wa Azovstal iliyoendeshwa na Umoja wa Mataifa na Kamati ya kimataifa Msalaba Mwekundu, ICRC, Bwana Awad amesema “hadi sasa hatujapokea ombi lolote lingine la kuhamisha raia kama lile la kule Mariupol. Lakini tunaendelea kuwasilisha maombi yetu ili kufikia maeneo ambako raia wanahitaji chakula, dawa na aina nyingine za misaada.”

Mama na mwanae waonana baada ya mwezi mmoja mbele ya nyumba yao iliyoharibiwa Chernihiv, Ukraine.
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Mama na mwanae waonana baada ya mwezi mmoja mbele ya nyumba yao iliyoharibiwa Chernihiv, Ukraine.

Ujumbe wake kwa pande zote

“Ujumbe wangu ni kwamba vita hii lazima ikome. Takribani nchi 69 zinaweza kuathiriwa na uhaba wa chakula, mfumuko wa bei, kuporomoka kwa mnyonyoro wa usambazaji bidhaa, ukosefu wa ajira na mambo mengine mengi,” amesema Bwana Awad.

Mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema tayari dunia inakabiliwa na changamoto nyingi. Mojawapo ni mabadiliko ya tabianchi ambayo inaathiri pia kilimo na vyanzo vingine vya kujipatia kipato.

“Kwa mtazamo wowote wa vita hii, kimkakati, kisiasa au kiuchumi, vita ni ubaya,” ametamatisha Bwana Awad akisema kuwa hakuna yeyote anayenufaika bali kila mtu anagharimika na anapoteza.