Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kupanda bei ya chakula na kushuka thamani ya sarafu ni mzigo mara mbili

Mkimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati anayeishi Cameroon akiwaandalia wateja wake chakula.
UN Women/Ryan Brown
Mkimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati anayeishi Cameroon akiwaandalia wateja wake chakula.

Kupanda bei ya chakula na kushuka thamani ya sarafu ni mzigo mara mbili

Ukuaji wa Kiuchumi

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Biashara duniani, UNCTAD hii leo imetoa ripoti ya tathmini ya athari inayoweza kutokea baada ya bei ya ngano kupanda wakati huo huo thamani ya sarafu ikizidi kushuka na kusema hali hii ni mzigo mara mbili. 

Taarifa iliyotolewa leo na UNCTAD kwa waandishi wa Habari mjini Geneva Uswis imeeleza kushuka huko kwa thamani kunaathiri nchi zinazo agiza chakula na nyingi ni zile zinazoendelea.

Tathmini hiyo pia imeeleza kwa mwaka huu wa 2022 bei ya chakula imeongezeka kila mahali, na kufikia viwango vya kihistoria.

UNCTAD imeeleza “Tathmini ya sasa ni tofauti na matatizo ya awali ya chakula, kwani sasa wananchi wanakabiliwa na mzigo maradufu kwani sio tu kwamba wanalipa bei ya juu kwa chakula wanachoagiza kutoka nje, lakini ongezeko la bei linachochewa zaidi na kushuka kwa thamani ya sarafu yao dhidi ya dola ya Marekani.”

Changamoto hizo mbili zinapunguza nafasi ya kifedha ambayo nchi nyingi zinazoendelea zinahitaji ili ziwezw kukabiliana na changamoto zinazofanana za madhara yaliyo sababishwa na janga la COVID-19, kupanda kwa gharama za maisha, na dharura zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.